Katibu Mkuu wiazara ya maliasili na utalii ,Dokta Franscis Michael akizungumza jijini Arusha.
Mwenyekiti wa kamisheni ya utalii Zanzibar, Rahim Bhaloo akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha .
…………………………………………..
Happy Lazaro,Arusha
Katibu mkuu wa wizara ya maliasili na utalii Dokta Franscis Michael amezindua rasmi kamati ya maandalizi ya mkutano wa 65 wa shirika la utalii duniani -kamisheni ya Afrika (65 UNWTO -CAF) Jijini Arusha leo,huku akiitaka kamati hiyo kuchukulia umuhimu na uzito majukumu waliyonayo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo , Dkt Fransis amesema kuwa ,wana sababu zote za kujivunia Tanzania kupata fursa ya kuandaa mkutano huo utakaofanyika tarehe 5 ha7 October ambao pia utatoa fursa ya kuitangaza nchi kwani utaleta watu wengi ambao watakuja kushuhudia yale yaliyotangwaza na Rais Samia Suluhu katika filamu ya Royal Tour hivyo ni vema wanakamati wakapangilia mambo yote mapema.
“Tumejaribu kutafuta watu kutoka katika nyanja, wizara zote katika kamati hii ili kusudi tuweze kuhakikisha kwamba maandalizi haya yanakuwa bora na yanafana na kuweza kufanya mkutano huu kuwa wa mfano,”amesema Dkt Fransis.
Amefafanua kuwa ,majukumu makubwa ya kamati hiyo ni kuandaa mkutano ambapo unatakiwa uweze kufana na kuwa kivutio kikubwa kwa watu wa nje na mataifa mengine kuja kutembelea nchi ya Tanzania.
“Tunatakiwa tuhakikishe kuwa kamati inafanya kazi kwa weledi kwasababu mkutano huu ni wa kimataifa, tunaleta viongozi wa nchi na nchi zingine hivyo ni lazima tuhakikishe Tanzania tunakuwa mfano wa kuigwa na nchi zingine,”ameeleza.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TTB , Felix John ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa kamati hiyo kutoka Tanzania bara amesema kuwa, tukio hilo wanalichukulia kimkakati kwasababu ni tukio ambalo linakwenda kuwaleta wageni wengi katika nchi.
“ni sehemu ya utekelezaji kwa vitendo katika mkakati wetu wa utalii mkutano ambao unalenga watalii wengi na wageni kuja katika nchi yetu kama mnavyofahamu mkutano huu utawakutanisha mawaziri wanaosimamia sekta ya utalii na uhifadhi kutoka nchi zote barani Afrika lakini pia watakuja na watu wengi hivyo wadau wetu muhimu wa sekta ya utalii wajiandae kupokea idadi kubwa ya wageni kutoka mataifa yetu ya Afrika,” ameseema Felix.
Naye Mwenyekiti wa kamisheni ya utalii Zanzibar ,Rahim Bhaloo amesema kuwa Tanzania imejifungua katika sekta ya utalii,kwani Rais Samia Suluhu ameitangaza sana vilivyo kwa kushirikiana na Rais Hussein Mwinyi ambapo ni fursa kwa Tanzania kujiuza kwa dunia kwa kujitangaza na kuonesha vivutio.
“ni muda wa kuamka na ni lazima washirikiane wote kwa pamoja kwani hizi ni fursa ambazo zitakuwa na fursa kwa watanzania hasa wananchi wa chini ambao wapo moja kwa moja katika sekta ya utalii hivyo waitumie fursa hiyo kujiletea maendeleo kama nchi na kama watanzania,” amesema Bhaloo.