Katibu Tawala (DAS) wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Winfrida Funto, akizungumza na wakina mama waliofika kwenye uzinduzi huo (hawapo pichani)
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Dk. Anthony Mwangolombe, akizungumza kwenye uzinduzi huo. |
Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya hiyo, Oliva Njoka. akitoa taarifa ya zoezi hilo la chanjo.
Godliver Mtasa akisoma taarifa ya uzinduzi wa kampeni hiyo ya chanjo ya polio.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ikungi aliyefahamika kwa jina moja la Athumani akizungumza kwenye uzinduzi huo. |
Muuguzi wa Zahanati ya Wilaya ya Ikungi, Edna Msangi akimpa tone la chanjo ya polio mmoja wa watoto wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo.
Wanawake wakiwa na watoto wao kwenye uzinduzi huo.
Uzinduzi ukiendelea.
Uzinduzi ukifanyika.
Wanawake wakiwa na watoto wao kwenye uzinduzi huo.
Mwanaume pekee Yasin Ibrahim aliyefika ili kupata chanjo mtoto wake Ally Yasin wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo. Hongera sana Yasin wanaume igeni mfano huo.
Viongozi na watumishi wa Zahanati ya Ikungi wakiwa kwenye uzinduzi huo.
Katibu Tawala (DAS) wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Winfrida Funto, akimpaka wino kwenye kucha mmoja wa watoto aliyepatiwa chanjo ili kuthibitisha kuwa tayari kapata chanjo hiyo.
Katibu Tawala (DAS) wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Winfrida Funto, akiwa amembeba mtoto baada ya kupatiwa chanjo hiyo.
Muuguzi wa Zahanati ya Wilaya ya Ikungi, Edna Msangi akimpa tone la chanjo ya polio mmoja wa watoto wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo.
Katibu Tawala (DAS) wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Winfrida Funto, akimpaka wino kwenye kucha mmoja wa watoto aliyepatiwa chanjo ili kuthibitisha kuwa tayari kapata chanjo hiyo.
Wanawake wakisubiri watoto wao kupatiwa chanjo.
Na Dotto Mwaibale, Singida
KATIBU Tawala (DAS) Wilaya ya Ikungi wa Mkoa wa Singida, Winfrida Funto ameongoza uzinduzi wa kampeni ya siku nne ya chanjo ya matone ya polio kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.
Kampeni hiyo ya siku nne ilianza jana Mei 18 na inatarajiwa kumalizika Mei 21 mwaka huu ambapo kimkoa ilizinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk.Binilith Mahenge Kata ya Iguguno wilayani Mkalama.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo Funto alisema mpaka leo Mei 19, 2022 tayari watoto 18, 060 walikuwa wamekwshwa pata chanjo hiyo na zoezi la uchanjaji likiendelea huku malengo yakiwa ni kuwafikia watoto 62,155.
Funto alisema chanjo hiyo inatolewa bure na kwamba zoezi hilo litakuwa la siku tatu na kuwa watahakikisha wanawafikia watoto wote waliopo wilayani humo na kuwa litafanyika nyumba kwa nyumba .
Alisema zoezi hilo ni la kitaifa hivyo hata kama hapo awali watoto walikwisha pata chanjo hiyo wanatakiwa kurudia tena kutokana na kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa huo nchini Malawi ambapo mtoto mmoja amebainika kuwa nao.
Alisema kutokana na ujirani uliopo baina ya Tanzania na nchi hiyo ukizingatia kuwa nchi yetu sio kisiwa ambapo kunaweza kuwepo kwa viashiria vya ugonjwa huo ndio maana Serikali imeamua kutoa kinga ya ugonjwa huo.
“Madhara ya ugonjwa wa Polio ni ulemavu wa ghafla wa viungo na usiotibika kwa hiyo ni muhimu sana kwa kila mzazi na mlezi kuhakikisha mtoto wake mwenye umri huo anapata chanjo hii ambayo ni salama baada ya kuthibitishwa na wataalam” alisema Funto.
Funto alitumia nafasi hiyo kumpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Justice Kijazi na Idara ya Afya wilayani humo kwa uhamasishaji wa zoezi hilo ambao umeleta hamasa kubwa kwa wananchi na kujitokeza kuwapeleka watoto wao kupata chanjo hiyo.
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Dk. Anthony Mwangolombe aliwaomba wazazi kutoa ushirikiano kwa kuwatoa watoto wao ili kupata chanjo hiyo kwani ni muhimu kwa uhai wa watoto ambao ni taifa la baadae.
Alisema mtoto anapokuwa ameathiriwa na ugonjwa huo changamoto hiyo haitaishia kwake tu bali na kwa mzazi ambaye atakuwa akitumia muda mwingi kumsaidia na kushindwa kufanya shughuli zingine za kiuchumi.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo Oliva Njoka alisema katika kutekeleza kampeni hiyo ya kitaifa ya chanjo hiyo wamejipanga kuchanja watoto 62,155 ambao wapo chini ya miaka mitano (Miezi 0-59) ambao ndio walengwa wa zoezi hilo.
Alisema zoezi hilo limefadhiliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Watoto Duniani (UNICEF) ambapo fedha zilizotengwa jumla ni Sh.105,869,783.67 huko UNICEF wakitoa Sh.37,957,616.67 sawa na asilimia 36 na WHO wakitoa Sh.67,912,167 sawa na asilimia 64. ya bajeti ya fedha zilizotengwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ikungi aliyefahamika kwa jina moja la Athuman akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kata hiyo aliishukuru Serikali kwa zoezi hilo na akatoa angalizo kwa watu wote wanaopotosha kuhusu zoezi hilo kuwa chanjo hiyo si salama kuwa wapuuzwe kwani hakuna Serikali ambayo inaweza ikaendesha zoezi la chanjo kwa lengo la kuwaathiri wananchi wake.
Kampeni hii inafanyika nchi nzima baada ya Serikali ya Malawi kutoa tamko mapema mwaka huu la kuwepo mlipuko wa Polio katika nchi hiyo baada mtoto mmoja kudhibitika kuwa na Polio na hivyo kuwa ni mara ya kwanza kwa bara ya Afrika kutokea changamoto hiyo baada ya kupita miaka mitano pasipo kuwepo na ugonjwa huo.