Na Mwandishi Wetu, Tabora
Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uuenezi, Shaka Hamdu Shaka ametembelea maskani iitwayo Lumbesa, inayoundwa na waendesha maguta na mikokoteni katika Barabara ya Ujiji Manispaa ya Tabora.
Akiwa hapo jana asubuhi, aliungana na wananchi wengine wakiwemo wazee kunywa kahawa na kubadilishana nao mawazo ya mambo mbalimbali na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya katika uongozi wake.
Shaka amewahamasisha vijana kuchapa kazi kwa bidii na kujiunga katika vikundi ili kurahisisha kufikiwa fursa mbalimbali hususan za mikopo.
Amesema endapo kila kijana ataamua kufanyakazi na kushiriki shughuli za uzalishajimali kwa jasho lake, umasikini utaondoka.
Shaka amesema kuwa endapo kila kijana atajituma kwa bidii vijana watajikuta wakiishi bila utegemezi unaosababisha kukithiri malalamiko kwenye mitandao ya kijamii.
Wakitoa maoni yao katika mazungumzo hayo, baadhi ya wajasiriamali katika kikundi hicho, walipongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Onesmo Kilengawana alisema mwaka mmoja wa Rais Samia umeleta manufaa makubwa hususan katika Mkoa huo katika sekta mbalimbali ikiwemo ya elimu.
Hata hivyo, aliomba kuongezwa kwa fursa za mikopo ya wajasiriamali ili kuwaongezea uwezo wa kujiendeleza kiuchumi.
Kwa upande wake, Bora Matawala anayejishughulisha na uuzaji viazi vya kuchemsha mihogo na karanga, alisema hatua ya Rais Samia kufanya ziara mkoani Tabora inaonesha jinsi anavyoupenda Mkoa huo na kuguswa na maendeleo ya wananchi.
“Nimefurahi kwa ujio wa Rais Samia Tabora, tutaendelea kumuunga mkono yeye na Chama Cha Mapinduzi,” alisema.