************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imetoa kipaumbele kikubwa cha ajira kwa watu wenye ulemavu, hivyo amewataka wajitokeze kwa wingi kuomba nafasi hizo mara yanapotolewa matangazo.
Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Mei 19, 2022) wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Stella Alex Ikupa katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Mbunge huyo alitaka Serikali inapotangaza nafasi za ajira itenge asilimia fulani kwa ajili ya wenye ulemavu tofauti na utaratibu uliopo sasa.
Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imeweka utaratibu maalumu wa uendeshaji wa michakato ya ajira katika Sekretarieti ya Ajira na kutoa upendeleo kwa watu wenye ulemavu pale zinapotangazwa ajira.
“Hata katika teuzi mbalimbali anazozifanya Mheshimiwa Rais Samia ametoa kipaumbele kwa watu wenye ulemavu. Hata hivyo watu wenye ulemavu wanapata fursa ya kwanza kwenye usaili wa ajira mbalimbali.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema katika kuhakikisha bandari za Mtwara na Tanga zinatumika ipasavyo, Serikali imeamua kutoa punguzo la asilimia 30 ya tozo katika gharama za kuhudumia shehena na meli kama sehemu ya mikakati ya kimasoko na kuvutia wateja kutumia bandari hizo.
Ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Nanyamba, Abdallah Chikota aliyetaka kujua Serikali ina mikakati gani ya kuwavutia wafanyabiashara wa Malawi, Zambia na Congo kutumia Bandari ya Mtwara na nchi nyingine ikiwemo Sudan Kusini na Uganda kutumia Bandari ya Tanga.
“Ni kweli kwamba serikali kupitia Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imetenga fedha kwa ajili ya maboresho ya bandari zetu zote nchini zilizoko ukanda wa bahari kuu na pia kwenye maziwa makuu kwa ajili ya kuimarisha miundombinu mbalimbali.”
“Tumeongeza vifaa vinavyoweza kupakia na kupakua mizigo kwa muda mfupi, pia tumepunguza tozo katika bandari za Tanga na Mtwara ili wateja wanaoleta mizigo katika bandari hizo na kuwahakikishia wateja upatikanaji wa huduma kwa muda mfupi zaidi.”
Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwakabirisha wafanyabiashara wa mafuta kutumia bandari hizo kwani licha ya kupunguza tozo, pia Serikali imefunga mita za kisasa za kupakua na kupakia mafuta ili kurahisha upakuaji na upakiaji wa shehena hiyo na wamejenga matenki ya kutosha.
Amesema Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) inatumia balozi zetu kuhamasisha wafanyabiashara wa huko kutumia bandari zetu na imefungua ofisi katika nchi za Congo, Malawi na Zambia ili wateja wanaohitaji huduma kupitia bandari zetu watapate mawasiliano wakiwa katika nchi zao bila ya kulazimika kuja Tanzania. Pia, amewahakikishia wafanyabiashara hao usalama wao na mizigo yao na kuwataka waendelee kutumia vema bandari zetu.
Amesema sambamba na maboresho hayo, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu mingine ya usafiri na usafirishaji hususan reli na barabara ili kuunganisha vema na majirani zetu hao kwa lengo la kuleta ustawi wa kibiashara na kiuchumi.