Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Godfrey Sanga akizungumza kwenye kikao kazi kilichowakutanisha watumishi 96 leo Alhamisi Mei 19,2022
Watumishi wa Ruwasa wakiwa kwenye kikao
Watumishi wa Ruwasa wakiwa kwenye kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano uliopo ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza
………………………………………….
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Katika kuhakikisha upatikanaji wa maji Vijijini unafikia asilimia 85 ifikapo mwaka 2025 Serikali kupitia Wakala wa maji na usafi wa mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoani Mwanza wamepanga kutumia shilingi bilioni 88 kukamilisha miradi ya maji Vijijini.
Akizungumza na Fullshangwe Blog mara baada ya kufungua kikao kazi cha watumishi wa Ruwasa Mkoa wa Mwanza, Meneja wa Ruwasa Mkoani humo Mhandisi Godfrey Sanga, amesema kuwa kwa sasa wanatoa huduma ya maji Vijijini kwa asilimia 67.
Amesema tayari wamesaini mikataba mipya ya miradi ya maji vijijini yenye thamani ya shilingi bilioni 88 ambayo itahudumia watu wote wa vijijini kwa asilimia 25 ambapo jumla itakuwa asilimia 92 ifikapo mwaka 2023.
“Tuko kwenye usanifu wa miradi mingine miwili ya mwisho ambayo itatumia zaidi bilioni 20 ambayo itaongeza maji kwa asilimia tatu, hivyo ninaamini hadi ifikapo mwaka 2025 Mkoa wa Mwanza utakuwa na zaidi ya asilimia 93 ya huduma ya maji vijijini ambapo itakuwa imepita malengo ya chama cha mapinduzi(CCM) ambayo inatutaka tufikishe maji kwa asilimia 85 Vijijini ifikapo mwaka 2025”,amesema Sanga
Sanga amewaasa wananchi waendelee kutunza vyanzo vya maji ili waweze kuwa na uhakika wa kupata maji safi na salama hali itakayosaidia kuepukana na magonjwa mbalimbali.
Kwa upande wake Afisa utumishi wa Ruwasa Mkoa wa Mwanza Zubeda Namaleche, amesema wamekuwa na utatatibu wa kukutana na watumishi wote kwa ajili ya kukumbushana maadili ya utumishi wa umma,utendaji kazi na kuonyana mambo mbalimbali ambayo yanakuwa hayaendi vizuri.
Ameongeza kuwa watumishi wafanye kazi kwa uaminifu na weledi mkubwa katika kutekeleza miradi hiyo na kuondoa tamaa ya kufanya ubadhilifu wa fedha za Serikali ambazo zinatolewa kwa ajili ya kuwasaidia wananchi kupata huduma ya maji safi na salama.
Frankson Kanyere ni mtumishi kitengo Cha fundi sanifu Mkuu kutoka Ruwasa Wilaya ya Misungwi amesema ukosefu wa vyombo vya usafiri imekuwa ni changamoto kubwa Hali inayopekekea kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa wakati na kuiomba Serikali kuongeza vifaa hasa magari ili kuwafikia wateja wengi kwa urahisi Vijijini.