Adeladius Makwega-WUSM
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini ndugu Haji Janabi amesema kuwa milango ya wizara hii ipo wazi kwa kila Mtanzania kufika kuzifahamu kwa kina sekta zinazosimamiwa na wizara hiyo.
Ndugu Janabi ameyasema hayo Mei 18, 2022 Mtumba-Mji wa Serikali Jijini Dodoma wakati akizungumza na wakaguzi wa nje kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wakiwa pamoja na wakuu wa idara na vitengo wa wizara hiyo katika kikao maalumu cha ukaguzi wa mali za zamani za serikali.
“Wizara yetu tunajishughulisha kwa kina na Utamaduni wetu, Sanaa yetu na Michezo yetu na ndiyo maana hapa ninao wakurugenzi wote wa sekta zetu, wapo pamoja na wakuu wa vitengo ili watoe ushirikiano kwa kila litakalo hitajika na kuulizwa tangu mwaka 2011 hadi sasa kwa mali hizo za zamani.”
Aliongeza kwa kuwa zoezi hilo limepitia hatua mbalimbali ana hakika linafanyika na litakamilika kwa ufanisi mkubwa.
“Ukiona ngoma makao makuu hapa, ukiona muziki makao makuu hapa hapa na hata ukiona michezo makao makuu hapa, karibuni pia kujifunza haya mambo yetu njia ni nyeupe na mlango umefunguliwa kwenu na kwa kila Mtanzania.”
Kaimu Katibu Mkuu Janabi ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Sera na Mipango wizarani hapa aliongeza kuwa wizara hii katika kutekeleza majukumu yake kikamilifu kimuundo imegawanyika katika maeneo makuu mawili moja ni usimamizi na utekelezaji wa masuala ya kisekta na pili ni uendeshaji, uratibu na usimamizi.
Kikao hicho kilikamilika kikamilifu na kutoa wasaa kwa wakaguzi hao kufanya kazi yao na wakuu wa idara na vitengo wizarani hapa kutoa ushirikiano na kujibu litakalo ulizwa.