**************************
Na Mwandishi wetu, Mirerani
WACHIMBAJI wa madini nchini wametakiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23 mwaka huu ili kujua idadi yao.
Katibu mtendaji wa Tume ya Madini mhandisi Yahya Samamba ameyasema hayo mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara kwenye mafunzo ya wachimbaji madini ya usalama, utunzaji mazingira na usimamizi wa baruti migodini.
Mhandisi Samamba amesema wachimbaji washiriki sensa ipasavyo ili Wizara ya Madini wafahamu idadi ya wachimbaji Tanzania ili kutambua namna ya kuwafikia.
Amesema wakifahamu idadi ya wachimbaji madini nchini kupitia sensa wataweza kutambua namna ya kuweza kuwafikia na kupambana na changamoto zao.
“Kupitia kupitia sensa hiyo ya watu na makazi, sekta ya madini tutatambua idadi ya wachimbaji na uwiano wa watumishi wa Tume,” amesema mhandisi Samamba.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Dk Suleiman Serera amesema suala la kushiriki sensa ya watu na makazi ni la kila mmoja hivyo watu wote wanapaswa kushiriki.
“Ni muhimu kila mtu ahesabiwe kwani tukipata idadi kamili ya watu nchini, tutaweza kupanga vizuri mipango yetu ya maendeleo,” amesema Dk Serera.
Amesema serikali inapaswa kufahamu idadi ya wananchi wake ilionao ili washiriki kuwahudumia kwenye sekta mbalimbali ikiwemo za afya, elimu na mengine.