Na Dotto Mwaibale, Singida
SINGIDA Golden Marathon yazinduliwa rasmi mkoani hapa huku siku ya kwanza ikiwa na mwamuko mkubwa wa wananchi kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya Peoples kwenda kushiriki.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika juzi Mwenyekiti wa Kamati ya Singida Golden Marathon ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya Singida Golden Runners , Raymond Msangi alisema Singida kumekucha kwa maandalizi ya Singida Golden Marathon ambayo itafanyika July 23, 2022 na kuwa hiyo ni nafasi ya kipee kama mwana Singida na Mtanzania kushiriki katika tukio hilo kubwa la kuhamasisha watu kufanya mazoezi huko dhamira kubwa ikiwa ni kusaidia afya ya mama na mtoto.
” Hatuwezi kufanya jambo ili peke yetu bila ya kuwaleta wadau pamoja kwa kufanya mazoezi na kuwashirikisha na wawe na tabia ya kufanya mazoezi ndio maana leo kwa mara ya kwanza tumeona tuzindue Singida Golden Runner ili kuleta ushirikiano wa pamoja kwa kufanya mazoezi na kujiandaa kwa Singida Golden Marathon” alisema Msangi.
Akizungumzia usajili alisema tayari umeanza na unafanyika kupitia http://singidagoldenmarathon.fasthub.co.tz na malipo yanalipiwa katika Akaunti namba 0131112000059 Banki ya NBC na kuwa unakwenda vizuri kufuatia wakimbiaji wengi kujitokeza kushiriki kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Singida.
Alisema zawadi zitatolewa kuanzia mshindi wa kwanza hadi wa 10 kutokana na kilometa 10 hadi 21 lakini zawadi hizo watazitangaza baadae.
Katibu wa Golden Brothers ambao ndio waratibu wa mbio hizo Omari Mtaturu alisema alisema mbio hizo zitakuwa ni za kipekee kwa kutizama tu hasama iliyojitokeza kwa siku ya kwanza ya uzinduzi wa kufanya mazoezi ambapo alilishukuru jeshi la polisi na wadau wengine, na vikundi mbalimbali vilivyojitokeza kushiriki uzinduzi wa mbio hizo.
Alisema katika mbio hizo wanategemea kuwa na washiriki zaidi ya 2000 lakini mpaka wakati uzinduzi huo ukifanyika tayari washiriki zaidi ya 800 wamekwisha jisajili.
Mmoja wa washiriki wa uziduzi huo Haika Masawe kutoka Wilaya ya Ikungi alisema mazoezi hayo ya awali kuelekea Singida Golden Marathon ni ya muhimu sana na akatumia nafasi hiyo kuwashukuru waandaaji na kuwa wameanza kwa kukimbia kilometa tano na kueleza ni jambo jema ukizingatia kuwa siku hizi watu wengi wanashambuliwa na magonjwa sugu yasioambukiza hivyo kufanya mazoezi ni tiba ya magonjwa hayo.
” Wito wangu kwa wananchi wa Mkoa wa Singida ni kuwaomba wajitokeze kwa wingi Jumamosi ya wiki hii kufika kwenye mazoezi hayo yatakayokuwa yakiendelea katika viwanja hivi vya Peoples hadi siku ya kilele ambayo itakuwa ni July 23, 2022″ alisema Haika.