************************
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
Mei 18
Jumla ya watoto 200,967 waliochini ya miaka mitano mkoani Pwani wanatarajia kupata chanjo ya matone (POLIO) ili kuwajengea kinga na kuzuia kuenea kwa virusi hivyo .
Hatua hiyo imekuja ,kufuatia february17 mwaka huu nchi ya Malawi kutoa tamko la kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa huo , baada ya mtoto mmoja kutoka Mji Mkuu wa Lilongwe kuthibitika kuwa na ugonjwa huo.
Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake,alisema kampeni hiyo Ni ya nyumba kwa nyumba ,itaanza Mei 18 hadi Mei 21 ndani ya mkoa huo.
Alibainisha, watoto wote chini ya miaka mitano watapata chanjo hii bila kujali kama walishapata chanjo katika ratiba zao za kawaida ya chanjo.
Aliitaka ,jamii itambue usalama wa chanjo hiyo na wasiingie katika upotoshaji wowote kwani Ni Kama chanjo nyingine.
Vilevile alisema kuwa ugonjwa huo hauna tiba ila hukingwa na chanjo ya Polio ambayo ipo katika mfumo wa matone .
“Nchi ya Malawi na Tanzania kuna mwingiliano mkubwa wa kibiashara na huduma nyingine za kijamii hivyo hatari ipo na chanjo ni muhimu itasaidia kuzuia ugonjwa huo usienee ;”
Kunenge alisema, chanjo ni ileile inayotumika miaka yote lengo ni kuongeza kinga , kuzuia mlipuko na kudhibiti watoto wasipatwe na virusi vya ugonjwa huo.
Alieleza , kwa mara ya mwisho Tanzania ilipata mgonjwa wa Polio Julai 1996 hivyo kampeni hii inatarajiwa kufanyika katika nchi zinazopakana na Malawi ikiwemo Zambia,Msumbuji, na Zimbabwe .
Mkuu huyo wa mkoa ,aliitaka jamii kuipokea kampeni hii na kutokuwa na hofu .
Ugonjwa wa polio unasababishwa na kirusi cha polio ambacho huambukizwa kutoka kwa mtu alieathirika kwenda kwa mwingine kwa kunywa au kula chakula ama kinywaji kilichochafuliwa na kinyesi chenye vimelea vya ugonjwa wa polio.
Virusi vya polio huzaliana katika utumbo na huweza kuathiri mfumo wa fahamu ikiwa ni pamoja na kupooza kwa ghafla kwa viungo ndani ya masaa machache hata kupelekea kifo .