Na John Walter-Monduli
Kituo cha Huduma ya mtoto na kijana kupitia shirika la Compassion Tanzania katika klasta ya Mti mmoja wilayani Monduli mkoani Arusha, kimetoa msaada wa magodoro 118 ili kusaidia huduma ya malazi kwa watoto na wajawazito wanaoishi katika mazingira Magumu.
Akikabidhi msaada huo Katibu tawala wilaya ya Monduli Robert Amosi amesema kilichofanywa na kituo hicho ni jambo la kuigwa kwa kuwa wengi wanaishi katika mazingira magumu na wanahitaji misaada ya namna hiyo na mingine zaidi.
Amesema shirika la Compassion katika wilaya ya Monduli ni wadau wakubwa wa Maendeleo likiwemo suala la kupiga vita vitendo vya kikatili.
Amosi amewasihi watoto katika kituo hicho kuwaheshimu wazazi wao na walimu wanaowafundisha na kuzingatia masomo ili kutimiza ndoto zao.
Akitoa shukrani zake, kwa niaba ya wazazi, mkazi wa Mti mmoja Grace Malasek amesema kabla ya kituo hicho watoto wengi walikuwa wakichunga mifugo na kukosa haki yao ya kupata elimu.
Amesema kwa magodoro waliyoyapata yatawasaidia kwa kuwa walikuwa wakitumia vitanda vya asili vinavyotumia ngozi.
Kwa mujibu wa Mratibu wa kituo hicho Lomnyaki Kispan mpaka sasa wana watoto 25 ambao wapo katika ngazi mbalimbali za elimu.
“Kwa kutambua kuwa wananchi wa mti mmoja ni sehemu ya jamii ya Wana Monduli, tumeona tuchangie kwa kutoa magodoro hayo ili walale sehemu nzuri na tuliwatembelea katika maeneo yao na kuona uhalisia” alisema Kispan.
Mmoja wa wanafunzi wa kituo cha ELCT Mti mmoja namba TZ 273 Jesca Petro, ameshukuru kwa kupatiwa msaada huo akieleza kuwa baadhi yao walikuwa wakilalia ngozi.