Asila Twaha, Kaliua
Washiriki wa Mafunzo Endelevu Kazini MEWAKA wameiomba Serikali kuendelea kuvisimamia na kuviwezesha vituo vya MEWAKA katika shule ili viweze kufanya kazi kwa ufanisi na kwa kupitia vituo hivyo walimu waeleze changamoto zao.
Hayo yamebainishwa na mshiriki wa mfunzo ya MEWAKA Mwl. Furaha Mwakasembe katika mafunzo yaliyofanyika hivi karibuni Mkoani Tabora Shule ya msingi Ushokola Halmashauri ya Wilaya ya Urambo lengo la mfunzo hayo likiwa ni kuwajengea uwezo walimu.
Mwakasembe amesema, pamoja na kuchelewa kwa mafunzo hayo wanaishukuru Serikali kuona ni muhimu walimu kupatiwa mafunzo kwa lengo la kuwajengea uwezo na jinsi ya kuviendeleza vituo vya MEWAKA mashuleni.
Aidha, amesema walimu itawasaidia kujifunza, kutatua changamoto na kupata maarifa mapya wanapokutana watabadilisha uzoefu na kushauriana sababu kazi ya ualimu kila siku unatakiwa uwe na mbinu mpya za ujifunzaji na ufundishaji.
Hata hivyo, pamoja na mafunzo haya kuendelea ambapo kila shule imepata nafasi ya ushiriki wa walimu wawili mwalimu wa taaluma na mwalimu mahiri amesema wakimaliza mafunzo hayo wanaenda kuwa mfano na viongozi bora kwa walimu wenzao kuweza kushirikiana nao kwa yale walio fundishwa na kwa wanafunzi wao.
“Tunaiomba Serikali kuendele kuviwezesha na kuvipa nguvu vituo vya MEWAKA katika suala la usimamizi wa kufuata sheria, taratibu na miongozo ili visije vikasimamishwa amesema.
Ili Serikali ipate maendeleo katika uboreshaji wa elimu nchini ni lazima vituo hivyo kuvisimamia sababu vitawasaidia kujua changamoto za elimu nchini” amesema Mwakasembe
Aidha, ameiomba Serikali kuendelea kuisimamia sekta ya elimu kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu ikiwa wao walimu wa shule za awali na msingi ndio msingi elimu wapo tayari kuendelea kutoa elimu bora kwa wanafunzi waliopewa jukumu la kuwasimamia.
Naye Mwl. Levina Mwanchang’a mshiriki wa mafunzo (Shule ya Msingi Senga) amesema, mwanzo walikuwa wanafundisha kwa uzoefu mwalimu hana mbinu mpya za kufundishia bila kujua kuna mabadilko katika ujifunzaji na ufundishaji kwa kupata mafunzo hayo yanaenda kuwasaidia kuongeza ujuzi na maarifa.
“Sio lazima uwe na nakala ngumu ndio uweze kupata materials unaweza kupata mbinu za kufundishia hata ukiwa na simu janja yenye uwezo wa kupata mtandao kuweza kupakua vitabu mbalimbali kutoka kwenye taasisi zetu za elimu na kupata “materials” yote haya tumeyapata kwenye mafunzo ya MEWAKA” amesema Mwl. Mwanchang’a
Kwa upande wa Mratibu wa Halmashuri ya Wilaya ya Kaliua Mwl. Matuna Massati amesema, jumla ya washirki 226 wameshiriki na tathmini wanayoendelea kuifanya baada ya mafunzo imeonyesha walimu wapo makini.
Kwa sababu mafunzo yanayoendelea ni kuwajengea uwezo katika utendaji kazi wao Serikali inaamini kumalizika kwa mafunzo hayo walimu wataenda kuwa viongozi bora katika utekelezaji wa kazi zao.