Picha ya mtandaoni ikimuonyesha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama akishiriki mjadala uliohusisha wadau mbalimbali katika kutathmini ongezeko la mshahara kwa asilimia 23.3 na maboresho ya masilahi ya watumishi wa umma.
*********************
Na. Veronica E. Mwafisi-Dodoma
Tarehe 17 Mei, 2022
Viongozi wa dini mbalimbali nchini wameupongeza uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wa kuridhia pendekezo la nyongeza ya mshahara wa kima cha chini kwa asilimia 23.3 kwa watumishi wa umma.
Viongozi hao wa dini wametoa pongezi hizo katika mjadala wa mtandaoni uliohusisha wadau mbalimbali katika kutathmini ongezeko la mshahara kwa asilimia 23.3 na maboresho ya masilahi ya watumishi wa umma yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita.
Askofu wa Dayosisi ya Karagwe, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Benson Bagonza amempongeza Mhe. Rais kwa uamuzi huo muhimu ambao utajenga ari ya utendaji kazi kwa watumishi wa umma.
Askofu Bagonza amesema dhamira ya Mhe. Rais ni ya kupongezwa na kuungwa mkono na Watanzania wote kwani watumishi wa umma ni kiungo muhimu kwani wanatoa mchango katika ujenzi wa uchumi wa Taifa.
“Dhamira ya Mhe. Rais kulitazama suala la nyongeza ya mshahara inalenga moja kwa moja kutekeleza dhamira yake ya kuhakikisha kwamba watumishi wanakuwa na ari ya kujenga uchumi wa nchi na ustawi wa Taifa,” Askofu Bagonza amesisitiza.
Kwa upande wake, Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania, Hemedi Jalala amesema ongezeko la mshahara na maboresho yaliyofanywa na Mhe. Rais katika utumishi wa umma yanadhihirisha namna serikali inavyowajali watumishi wake.
“Nina imani kuwa ongezeko la mshahara la asilimia 23.3 na maboresho mengine yaliyofanywa na serikali katika utumishi wa umma ni ishara ya upendo wa Serikali kwa watumishi wake,” Sheikh Jalala ameongeza
Awali, akieleza maboresho yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika utumishi wa umma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama amesema, azma ya Mhe. Rais ni kuhakikisha watumishi wanafanya kazi kwa bidii, weledi, uzalendo na kujituma bila kushurutishwa na ndio maana ametoa kipaumbele cha kuboresha masilahi ya watumishi.
“Kama Mhe. Rais amejitoa kikamilifu kuboresha masilahi ya watumishi wa umma nasi watumishi tunao wajibu wa kufanya kazi kwa bidii na uzalendo kwa ustawi wa Taifa letu,” Mhe. Jenista amehimiza.
Mjadala huo wa mtandaoni uliofanyika kwa zaidi ya saa mbili, uliandaliwa na Watch Tanzania News Agency na kuongozwa na Bw. Omari Kibanga.