*************
Na John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema kilele cha mashindano ya 67 ya UEFA baina ya Timu ya Real Madrid na Liverpool yataoneshwa mubashara nchini kwenye daraja jipya la Tanzanite jijini Dar es Salaam kupitia DStv ambapo vivutio mbalimbali vya utalii vitaonyeshwa moja kwa moja hivyo kutoa fursa kwa mamilioni ya wapenzi wa soka kutoka nchi zote za Afrika na dunia kushuhudia shindano hilo na vivutio vya utalii kutoka Tanzania.
Akizungumza kwenye kipindi cha Powerbreakfast kinachorushwa na kituo cha Redio cha Clouds Fm leo Mei 17, 2022 jijini Dar es Salaam. Mhe, Mchengerwa amesema mbali na kurusha mubashara mechi hiyo yenye mvuto mkubwa hapa nchini na duniani kote pia Filamu ya Royal Tour itaonyeshwa kabla ya kuanza kwa mechi hiyo ambapo ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kushuhudia tukio hilo la kihistoria.
Amefafanua kuwa wakati wa Filamu hiyo ya kihistoria iliyomshirikisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe Samia Suluhu Hassan ambayo imefungua Tanzania duniani, kutachezwa droo ambapo washindi watatu watakaopatikana watatembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini kwa ufadhili wa Bodi ya Utalii nchini(TTB) na Kampuni ya Heinken.
Aidha, amesema dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuendelea kutumia sekta za michezo na Sanaa kuitangaza Tanzania na vivutio vyake duniani kwa kuwa zimebeba idadi kubwa ya Tanzania na kuongeza kuwa sekta hizo ndiyo nguvu shawishi ya Serikali zinazowapa watanzania wengi zaidi furaha na faraja.
“Nipende kumpongeza Rais wetu kwa kazi kubwa sana na mikakati thabiti anayoifanya hivi sasa ya kuifungua Tanzania kupitia sanaa na michezo ambapo hivi karibuni ameandika historia kwa kushiriki moja kwa moja katika kuandaa filamu ya Royal Tour” ameongeza Mhe. Mchengerwa.
Ametaja baadhi ya mikakati mingine inayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano. Mhe Samia Suluhu Hassan kuifungua na kuitangaza Tanzania duniani kupitia Sanaa na michezo kuwa ni pamoja na kuandaa mashindano makubwa barani Afrika ya tuzo za wasanii ili yafanyike hapa nchini yanayojulikana kama MTV Afrika Awards hapo mwakani, kuandaa mkutano wa marais wa mashirikisho ya soka utakaohudhuriwa na zaidi ya nchi 54 za Afrika jijini Arusha ambapo Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) anatarajiwa kuhudhuria pamoja na kufikiria kuandaa mashindano makubwa ya soka Afrika kuanza kufanyikia hapa nchini.
Pia ameongeza kuwa tayari Serikali kupitia Wizara anayoiongoza inakamilisha michoro kwa ajili ya kujenga kumbi za kisasa za michezo na maonesho ya sanaa ambapo moja inatarajia kuchukua takribani watu elfu ishirini jijini Dar es Salaam na nyingine yenye uwezo wa kuchukua watu elfu kumi na tano jijini Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Heinken Nchini ambayo ndiyo mdhamini mkuu wa tukio hilo Bi Fatma Mnaro amefafanua kuwa lengo la kuonesha mubasha kilele cha UEFA hapa nchini kupitia DSTv ni kutaka kuwafanya wapenzi wa soka walione shindano hilo kwa ubora wa hali ya juu kama ambavyo watakavyoshuhudia wale ambao watahudhuria mtanange huo nchini Paris nchini Ufaransa.
Aidha, Bi. Mnaro ameongeza kuwa pamoja na kurushwa mubashara kwenye Daraja la Tanzanite pia kuna sehemu mbalimbali za majiji makubwa ambazo pia zitaonesha ambazo ni pamoja na The Cask jijini Mwanza, City Pub jijini Mbeya, Arusha na Capetown Fish Market, Samakisamaki na Triple 777 jijini Dar es Salaam.