Na Mwandishi wetu, Mirerani
SERIKALI imetoa shilingi bilioni 1 fedha za ujenzi wa soko la madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara hivyo ujenzi wake kuanza wakati wowote.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Dk Suleiman Hassan Serera ameyasema hayo mji mdogo wa Mirerani, kwenye mafunzo ya wachimbaji madini ya usalama, utunzaji mazingira na usimamizi wa baruti migodini ulioandaliwa na Tume ya Madini.
Dk Serera amesema Serikali imeshatoa shilingi bilioni 1 kati ya shilingi bilioni 5 zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa soko la madini kwenye mji wa madini Mirerani Tanzanite City.
“Wakati wowote wafanyakazi wa shirika la nyumba la Taifa (NHC) wataanza ujenzi wa soko hilo hivyo tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo za kuanzia ujenzi,” amesema Dk Serera.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, mhandisi Yahya Samanda akifungua mafunzo hayo amesema lengo la Serikali kuagiza madini ya Tanzanite yauzwe Mirerani ni kuhakikisha Mirerani inafanana na Tanzanite.
Amesema agizo la Tanzanite ichimbwe Mirerani, ikatwe Mirerani, isanifiwe na kuuzwa Mirerani ni kuhakikisha Mirerani inafanana na jiji la Arusha kiuchumi.
Katibu wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara (Marema) Tareq Kibwe amepongeza hali hiyo kwani itachangia kwa namna moja au nyingine uchumi wa wananchi wa Mirerani.
“Serikali ikiahidi jambo lake inatekeleza tunaipongeza sana kwa hatua hiyo kwani itakuwa fursa nzuri kwa wachimbaji madini na wadau wote wa madini,” amesema Kibwe.
Mjumbe wa MAREMA, Jafary Matimbwa amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuijali Mirerani na kufanikisha uanzishwaji wa ujenzi wa soko hilo.
“Mama Samia alifika mwaka jana mwezi wa Agosti kwenye kurekodi filamu ya Royal Tour akatuahidi ujenzi wa soko hilo na sasa fedha zimeletwa ujenzi utaanza,” amesema Matimbwa.