Dar es Salaam
Afisa wa Kanda wa Programu za Kiingereza (Regional English Language Officer – RELO) Bi. Diane Millar, anayesimamia programu ya Wizara ya Mambo ya Nje Marekani inayotoa mafunzo ya Kiingereza na kuwaendeleza walimu kitaaluma katika nchi 15 za Afrika Mashariki, alitembelea Tanzania kuanzia tarehe 5-15, 2022. Katika ziara hiyo, alikutana na viongozi wa serikali, viongozi wa taasisi za kielemu na vyama vya walimu. Aidha, alizindua programu mpya za mafunzo ya Kiingereza, aliendesha warsha za mafunzo kwa walimu na kuangalia matokeo ya programu za Marekani nchini Tanzania.
Akiwa Kigoma, Dodoma, na Pemba, RELO Bi. Millar alizindua programu mpya za mafunzo ya Kiingereza (English Access Microscholarship Program – Access) ambazo zitatekelezwa hadi mwaka 2024. Programu za Access huimarisha stadi za Kiingereza kwa vijana kutoka jamii masikini huku ikiwajengea uwezo katika stadi za uongozi na kuwa raia wanaowajibika. Kwa kawaida wahitimu wa programu hii huwa viongozi katika shule zao, hufanya vizuri zaidi katika mitihani yao na hupata fursa nyingi na nzuri zaidi za kujiendeleza kielimu. Wahitimu hawa, sio tu hupata kazi nzuri zaidi bali pia hutengeneza nafasi za kazi katika jamii zao! Hali kadhalika, washiriki wa programu hizi huwa na uwezo zaidi wa kushindania fursa za kushiriki katika programu za mabadilishano na masomo nchini Marekani. Nchini Tanzania, programu hizi zimeshafanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Unguja, Pemba, Mwanza, Tanga, Mbeya na Lindi zikitoa zaidi ya wahitimu 500.
RELO Millar alikutana pia na viongozi na wanachama wa Chama cha Walimu wa Kiingereza Tanzania (Tanzania English Language Association – TELTA) na Chama za Walimu wa Kiingereza Zanzibar (Zanzibar Professional English Language Teaching Organization – ZAPELATO) na kufanya nao kazi ya kuandaa na kuendesha warsha kwa walimu katika mikoa ya Kigoma, Dodoma, Unguja na Pemba. Pia aliwapatia taarifa kuhusu rasilimali na programu nyingi za bure ambazo walimu wanaweza kunufaika nazo.
Jijini Dar es Salaam, alikutana na wahitimu wa programu maalumu iitwayo Kinful program. Programu hii iliyoendeshwa na Ubalozi na kufadhiliwa na ofisi ya RELO, ililenga kuwajenga wanafunzi wa sekondari katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Mtwara katika stadi za kijamii na kujitambua (social-emotional learning), matumizi ya teknolojia za kidijitali, fikra na tafakuri tunduizi (critical thinking), uongozi na stadi za Kiingereza. Wahitimu walieleza jinsi programu hii ilivyowasaidia kuwa wanafunzi wazuri na wanaowajibika na kujituma zaidi. Walieleza kuwa programu hii imewafanya wawe viongozi wanaojiamini na wenye kujali hisia za wengine. Aidha walieleza jinsi programu hii ilivyowasaidia kuboresha stadi zao katika Kiingereza hususan katika kuzungumza na kusikiliza.
Katika ziara hiyo RELO Millar alikutana pia na maafisa wa Wizara ya Elimu na viongozi wa vyuo vikuu katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar na kuwajulisha kuhusu programu mbalimbali zinazoendeshwa na Serikali ya Marekani na kujadili kuhusu maeneo ya ushirikiano na yanayoweza kupatiwa misaada, hususan katika utoaji mafunzo na maendeleo ya kitaalamu ya walimu.