**************
SHULE ya Sekondari ya Ayalagaya iliyopo mkoani Manyara ambayo imeshika nafasi ya tatu kitaifa matokeo ya kidato cha nne mwaka 2021 wameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha miundombinu ya shule yao, hivyo kufanya shule kimasomo.
Wametoa salamu hizo za shukrani kwa Rais Samia na Serikali yake kupitia Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Shaka Hamdu Shaka ambaye alifanya ziara ya kuitembelea shule hiyo kwa lengo la kuwapongeza na kuwafikisha salamu za Rais Samia kuwa ataendelea kuboresha miundombinu ya sekta ya elimu nchini.
Mkuu wa Shule hiyo Stephene Naman amemueleza Shaka kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inastahili pongezi na shukrani kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya shule hiyo , hivyo kwa kipekee wanamshukuru Rais Samia.
“Taaluma ya wanafunzi shuleni kwetu imekuwa ikimarika na kuridhisha mwaka hadi mwaka kwani mwaka 2021 shule ilikuwa na ufaulu wa daraja la kwanza hadi daraja la tatu tu katika matokeo ya mtihani wa taifa kidato cha nne mwaka jana.
“Katika matokeo ya mtihani jumla ya wanafunzi waliofanya mtihani walikuwa 95, waliopata daraja la kwanza ni wanafunzi 29,daraja la pili wanafunzi 54 na daraja la tatu walikuwa 12.Hakuna daraja la nne wala zero.
“Kwa matokeo hayo tumefanikiwa kuwapeleka wanafunzi 83 ngazi ya kidato cha tano na wanafunzi 12 vyuo vya kati.Mafanikio yetu yanatokana na jitihada za Serikali kuboresha miundombinu yetu hapa shuleni,”amesema.
Akifafanua zaidi, amesema shule yao imepata tuzo mbili kutoka Wizara ya TAMISEMI kwa kushika nafasi ya tatu kitaifa kwa shule za kata na nafasi ya kwanza kwa shule zilizoboresha ufaulu kwa kiwango cha juu kwa miaka mitatu mfululizo.
Kuhusu hali ya ujenzi wa maabara, madarasa , mabweni na bwalo , Naman amemwambia Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM kuwa ujenzi wa madarasa mawili umekamilika na mradi umegharimu Sh.46,576,140 .
Pia wamekamilisha mabweni mawili kwa ajili ya kidato cha tano na sita yaliyogharimu Sh.425,960,262.Aidha ujenzi wa maabara mbili na darasa moja yaliyogharimu Sh.189,294,600 pamoja na ujenzi wa bwalo88 ambalo limegharimu Sh.248,960,651.