Baadhi ya washiriki kwenye warsha ya wakaguzi wa ndani iliyoandaliwa na Taasisi ya Ukaguzi wa Ndani nchini (IIA), ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Uelewa wa Wakaguzi wa ndani duniani. |
Mwandishi Wetu, Tanga
SERIKALI inategemea kuwa na Wakaguzi 300 wa Mifumo kote nchini katika sekta za Umma ifikapo Mwaka 2026 ili kuhakikisha inaweka udhibiti wa mapato kwenye shughuli zinazofanywa na taasisi zake mbalimbali.
Wakati huo huo imezitaka sekta binafsi kuhakikisha zinatambua umuhimu wa wakaguzi wa ndani na kuwajengea uwezo wakaguzi wao ili waweze kufanya ukaguzi wa mifumo kwa ufanishi, huku wakiwa na vyeti vinavyotambulika kimataifa.
Kauli hiyo, imetolewa juzi jijini Tanga na Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali, Bw. Athumani Mwituka alipokuwa akizungumza kwenye warsha ya wakaguzi wa ndani iliyoandaliwa na Taasisi ya Ukaguzi wa Ndani nchini (IIA), ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Uelewa wa Wakaguzi wa ndani duniani.
Katika warsha hiyo Serikali imeweka wazi mapungufu ambayo hung’amuliwa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG na nini kifanyike ili kupunguza hoja za mashaka ndani ya taasisi zao, amewataka wakaguzi hao kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni na miongozo ya kimataifa, hivyo wana kila sababu ya kuongeza ujuzi wao kwa manufaa ya taasisi na taifa kwa ujumla.
Alisema kwa kuanzia aupande wa Serikali imeanzisha mifumo mingi ya ukusanyaji mapato ambayo inachangia katika udhibiti matumizi mabaya na pia imechangia kurahisisha utendaji kazi wa shughuli zake.
” Upande wetu serikalini tumejipanga ifikapo Juni 2026 tuwe na wakaguzi wa mifumo kwa sekta za umma takribani 300. Tunatoa wito kwa sekta binafsi nao kuhakikisha inawajengea uwezo wakaguzi wao ili waweze kufanya ukaguzi wa mifumo kwa ufanishi, huku wakiwa na vyeti vinavyotambulika.
Serikali itaendelea kuongeza uwezo wa wakaguzi wa ndani ikiwemo kufanya ukaguzi wa miradi na tayari Waziri wa Fedha na Uchumi, ametoa maelekezo ya kuwa kila unapobuniwa mradi ndani ya taasisi zake itengwe fedha kwa ajili ya kufanikisha mkaguzi wa ndani kufanya ukaguzi wake.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya IIA, Bi. Zelia Njeza akizungumza alisema taasisi hiyo ya wakaguzi inaungana na wakaguzi wengine duniani kote kusherekea mwezi huu wa wakaguzi wa ndani, na umejipanga kusherehekea kitofauti zaidi kwa kuhakikisha tunawajengea uwezo wakaguzi wa ndani.
Alisema maadhimisho ya mwaka huu pamoja na kuwajengea uwezo wanachama wao, lakini wamelenga zaidi kujumuika na kusherekea mafanikio ya ukaguzi wao ndani ya taasisi wanazofanyia kazi.
Alisema bado kunachangamoto ya uelewa wa kazi za wakaguzi wa ndani katika jamii na changamoto hii ya uelewa haipo katika jamii ya Watanzania tu bali hata katika nchi zingine.
“…Kwa ujumla ukitofautisha na fani zingine kama udaktari, mtu yeyote ukimuuliza kuhusu daktari atakujibu ni nani…tumekubaliana mwezi huu wa tano uwe ni mwezi maalum kuweza kusherehekea mafanikio yoyote tuliyoyaleta kwa kutumia kazi zetu.
“…Na ni kipindi ambacho tunatumia fursa hii kuweza kuwaelimisha wadau wetu kuhusu umuhimu wa wakaguzi wa ndani na ni kitu gani wategemee kutokana na kazi zetu, kutoa elimu kwa wadau ni muhimu kwani kama hawatajua nini tunakifanya wanaweza wakawa na kigugumizi hata kuitaji huduma zetu,” alisema.