Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka akieleza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za NEMC leo Mei 16,2022 Jijini Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za NEMC leo Mei 16,2022 Jijini Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za NEMC leo Mei 16,2022 Jijini Dar es Salaam.
*********************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limesema kuwa hakuna athari zozote za kimazingira katika ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi eneo la Chongleani Mkoani Tanga kama ambavyo imekuwa ikidaiwa na baadhi ya wanaharakati.
Akizungumza Dar es Salaam leo Mei 16 Jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa NEMC Dkt. Samuel Gwamaka amesema taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari vya nje na wanaharakati hao zikilenga kupinga ujenzi wa bomba hilo, hazina ukweli wowote na kusisitiza kuwa zinapaswa zipuuzwe.
Amesema kabla ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo walihusishwa katika hatua zote za tathmini za kimazingira na kujiridhisha kuwa hakukuwa na athari zozote wakati wa maandalizi na utekelezaji wa mradi husika.
“Kimsingi tathimini ya kimazingira katika mradi huu ilifanywa kwa kuvihusisha vyombo mbalimbali vya Serikali na taasisi zote zinazohusika na mradi huo sambamba na wataalamu kutoka nje ya nchi hivyo ieleweke wazi kuwa mradi hui umezingitia matakwa yote kabla ya kuanza kwake” alisema DK Gwamaka
Aidha amesema tayari ujenzi wa bomba hilo umeanza kwa hatua za awali kwa maeneo ya kipaumbele ambapo wananchi wanaoguswa wanalipwa fidia na NEMC inafuatilia kwa karibu mradi huo na imeridhishwa na mwenendo wa mradi husika kuwa masharti yaliyowekwa yanafuatwa.
Pamoja na hayo amesema Baraza limekuwa likiendelea kufuatilia hatua mbalimbali za ujenzi wa bomba hilo kwa ajili ya kujiridhisha kama kilichoandikwa katika andiko la tathmini kinatekelezwa hatua aliyoisisitiza kuwa ni moja ya jukumu la NEMC.