Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Uongozi wa Kampuni ya Mamba Cement imekata mzizi wa fitina, baada ya kuamua kuwalipa fidia baadhi ya wakazi wa Magulumatali kata ya Talawanda , Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo ili kupisha ujenzi wa Kiwanda cha kutengeneza Saruji.
Fidia hiyo ni ya hekari 600 ikiwa ni sehemu ya ardhi ambapo baadae Kampuni hiyo itamaliza eneo jingine la hekari 600 zilizobaki.
Licha ya malipo hao mkazi Selemani Pendo na Mwajuma Mohamed walisema kuwa hatua hiyo imekuwa faraja kwao, kwani mgao wa fidia wa awali ulikuwa sio wa kuridhisha .
Mwajuma alisema kwamba hatua hiyo ya Kampuni hiyo kuwafanyia uhakiki kwa mara ya pili, inaonesha ni namna gani uongozi wake unavyojali na kuthamini ardhi ya wananchi hao waliokuwa wanaitumia kwa kilimo wengine wakiwa na makazi.
“Binafsi namshukuru Mwenyezi Mungu nimelipwa sidai tena, nawaomba wenzangu tuupatie ushirikiano viongozi waweze kufanikisha malengo ya ujenzi kwani tutapata ajira,” alisema Mwajuma.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho Mohammed Zikatimu alieleza, wakazi hao walifanyiwa uhakiki wa awali kisha kulipwa, lakini walipinga kiwango kidogo, ikarejewa uthamini hatimae wamewalipa wote.
“Kwa sasa katika hekari 600 za kwanza hakuna mkazi anayedai, ukiachilia hekari 600 zilizobaki ambazo uongozi wa Kampuni unatarajia kuendelea na mchakato wa kuhakiki kisha kuwalipa fidia zao,” alisema Zikatimu.
Diwani wa Kata hiyo Ramadhani Biga alisema kwamba zoezi hilo limekwenda vizuri, huku akiushukuru uongozi wa Kampuni kwa kumaliza sintofahamu hiyo iliyochukua miaka zaidi ya kumi.