Mkurugenzi wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia Zanzibar (KIST), Dkt. Mahmoud Abdulwahab, akizungumza katika Kikao cha pamoja kuhusu masuala ya Kidigitali baina ya Uongozi wa ICDL na Uongozi wa Taasisi ya Karume Sayansi na Teknolojia Zanzibar (KIST),hafla iloyofanyika Ukumbi wa Dokta Idrissa Muslim Hija katika Taasisi hiyo Mbweni Mjini Zanzibar.
Meneja wa ICDL Nchini Tanzania, Edwin Masanta, akielezea lengo kuu la Kikao cha pamoja baina ya Uongozi wa ICDL na Uongozi wa Taasisi ya Karume Sayansi na Teknolojia Zanzibar (KIST), huko Ukumbi wa Dokta Idrissa Muslim Hija katika Taasisin ya Karume Mbweni Mjini Zanzibar.
Wawakilishi kutoka Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Uelewa wa masuala ya Kidigitali (ICDL) wakielezea lengo la kufika katika Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia Zanzibar (KIST), kufanya majadiliano yatakoiwezesha Taasisi ya Karume kuwa kituo cha mafunzo ya Kidigital kwa upande wa Zanzibar.
PICHA NA MARYAM KIDIKO – KIST.
……………………………………………
Na Issa Mzee – KIST
Ujumbe kutoka Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Uelewa wa masuala ya Kidigitali (ICDL), umefika katika Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia Zanzibar (KIST), kwa lengo la kufanya majadiliano yatakoiwezesha Taasisi ya Karume kuwa ni kituo cha mafunzo hayo kwa upande wa Zanzibar.
Kikao hicho kilifanyika katika Ukumbi wa Dokta Idrissa Muslim Hija katika Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia (KIST) Mbweni Mjini Zanzibar, baina ya Uongozi wa ICDL na Uongozi wa Taasisi ya Karume Sayansi na Teknolojia Zanzibar (KIST).
Akizungumza katika kikao hicho Meneja wa ICDL Nchini Tanzania, Edwin Masanta, amesema lengo kuu la kuanzishwa kwa mafunzo hayo Zanzibar ni kuisaidia jamii kukuza na kupata uelewa wa hali ya juu katika masuala ya kidigitali ambayo yamekuwa yakitumika katika nyanja mbalimbali za maendeleo nchini.
Alisema kuwa, bado idadi kubwa ya watanzania hawana uelewa wa kutosha wa kutumia mitandao katika harakati zao za maendeleo hivyo ipo haja ya kukuza uelewa wao katika masuala ya mitandao ili waweze kujenga ufanisi utakao wawezesha kujua vyema matumizi ya mitandao katika shughuli zao za kila siku.
“Ipo haja ya kuwaandaa watanzania hasa wasomi kuwa na ujuzi wa hali ya juu katika masuala ya kidigitali mafunzo haya yatawasaidia wananchi waweze kuendana na ulimwengu wa sasa popote watakopoenda”, alisema Meneja huyo.
Alifafanua kuwa, endapo watu mbalimbali watajiunga na mafunzo hayo yatakayoendeshwa katika Taasisi ya Karume yatawawezesha kupata vyeti vya kimataifa ambavyo vitawasidia kutambulika kimataifa na kuweza kuajirika na kufanya kazi popote duniani.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia Zanzibar (KIST), Dkt. Mahmoud Abdulwahab, alisema mpango huo wa kutoa mafunzo ya kidigitali kwa watu mbalimbali Zanzibar ambao utasimamiwa na Taasisi yake utasaidia kutengeneza wataalamu wazuri wenye uwezo wa hali ya juu kitika masuala ya mitandao ambao wataweza kulisaidia taifa katika harakati za maendeleo.
“Hivi sasa dunia inaendeshwa kidigitali hivyo lazima watu wawe na uelewa wa hali ya juu katika masuala ya kidigitali, hivyo kwa upande wa Zanzibar Taasisi ya Karume ndio Taasisi pekee itakayoendesha mafunzo hayo na mitihani ya ICDL”, alisema Mkurugenzi.
Hata hivyo, alisema hivi sasa Taasisi ipo katika hatua ya kuandaa hati ya makubaliano ili mafunzo hayo yaanze kutolewa rasmi katika Taasisi hiyo.
Aidha alisema kufanyika kwa mafunzo hayo kutasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuitangaza Taasisi ya Karume na kukuza hadhi ya Taasisi Kitaifa na Kimataifa.