Kamishina wa fedha wa uchumi wa Jeshi la polisi Hamad Khamisi Hamad akizungumza wakati wa kufungua mkutano wa kimtandao ulioandaliwa na OJADACT
…………………………………………………..
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Kamishina wa fedha wa uchumi wa Jeshi la Polisi Hamad Khamis Hamad amesema hayo wakati akifungua mkutano wa kimtandao ulioandaliwa na chama cha waandishi wa habari wa kupiga vita matumizi ya Dawa za kulevya na uhalifu Tanzania(OJADACT) kwa kushirikiana na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) pamoja na Jeshi la Polisi Nchini.
Kamishina Hamad ameweka bayana kuwa lazima kuwe na mkakati wa pamoja baina ya jeshi la polisi na vyombo vya habari ili kuzuia uhalifu Nchini.
‘Vyombo vya habari vina nguvu na uharaka wa kuifikia jamii na endapo vikitumika vitasaidia sana kuzuia uhalifu.
David Misime msemaji wa Jeshi la Polisi amesema kuwa, vyombo vya habari viwekeze zaidi kwenye kutoa elimu ya athari za uhalifu kuliko kuripoti matukio.
“Tukiwekeza zaidi kwenye kutoa elimu itatusaidia sana kwenye kukabiliana na uhalifu bila kuathiri ushahidi wa kesi hii itatusaidia kulinda amani na usalama wa Taifa letu.
Onesmo Orengurumwa, Mratibu wa Mtandao wa watetezi wa haki za binadamu Tanzania amesema kuwa, matukio ya kihalifu yanayoendelea hapa Nchini yanavunja haki za binadamu kwani hakuna takwa la kisheria la kutenda uhalifu.
” Jeshi la Polisi lifanye kazi kwa ukaribu na waandishi wa habari na watetezi wa haki za binadamu kwenye kupambana na uhalifu mfano huu wa panya road” alisema orengurumwa.
Pia alisisitiza makundi yote ya kijamii yawe kitu kimoja kwenye kutafuta chanzo cha tatizo lolote kwa jicho la mbali hivyo jeshi la polisi lishirikiane na makundi yote kwa pamoja.
Naye Bi Christina Mwangozi Kaimu mkuu wa Kitengo cha habari wizara ya mambo ya ndani amesema kuwa, kwa sasa kuna matatizo makubwa ya kuripoti matukio ya kihalifu kwa hatua (series) ambayo yanaharibu upelelezi wa kipolisi na pia kuleta chuki kwenye jamii jambo ambalo halina tija.
” Endapo utatazama hizo series hadi mwisho ni wazi kuwa mhusika anaweza kuhamasika kutenda uhalifu kwani anavutiwa na jinsi jambo la kihalifu linavyoripotiwa.
Mwenyekiti wa OJADACT bwana Edwin Soko alisema kuwa, vyombo vya habari viepuke kuripoti zaidi badala ya kuelimisha jamii juu ya uhalifu.
Pia alisema kuwa, OJADACT inamshukuru sana Mkuu w Jeshi la Polisi Tanzania Simon Sirro kwa kukubali jeshi la polisi kukaa na waandishi na kujadili changamoto za kuripoti matukio ya kihalifu.