Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju akisalimiana na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa Happiness Seneda mara baada ya kuwasili mkoani humo kwa ziara ya siku mbili.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju akizungumza katika kikao na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mkoani Iringa akiwa ziarani mkoani humo.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Grace Mbwilo, akifafanua jambo katika kikao cha Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju na NGOs za Mkoa wa Iringa.
Washiriki wa kikao cha Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju na NGOs za Mkoa wa Iringa wakifuatilia maelezo ya Naibu Katibu Mkuu (hayupo pichani) katika kikao hicho.
Baadhi ya wadau wa NGOs wakichangia mawazo katika kikao cha Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju na NGOs za Mkoa wa Iringa.
Afisa Maendeleo ya Jamii Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa Saida Mgeni akieleza hali ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika mkoa huo wakati wa kikao cha Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju na NGOs za Mkoa wa Iringa.
……………………………………………..
Na WMJJWM, Iringa
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju ameyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) yapatayo 4909 nchini kuwasilisha maelezo ya kwanini yasifutiwe usajili kwa kukiuka sheria na taratibu zinazo yaongoza.
Mpanju ametoa agizo hilo alipokutana na NGOs za Mkoa wa Iringa katika ziara yake ya siku mbili mkoani humo yenye lengo la kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya Wizara.
Mpanju amesema kuwa, Mashirika hayo yameshindwa kutekeleza matakwa ya kisheria inayowataka kuwasilisha taarifa zao kwa ajili ya uhakiki, lakini tangu zoezi la uhakiki lianze mwaka jana mashirika hayo yameshindwa kufanya hivyo.
“Hadi zoezi linakamilika mwezi Machi mwaka huu ni Mashirika 4864 kati ya 12884 yamehakikiwa na mashirika 7533 ndiyo yapo hai baada ya zoezi la uhakiki, sasa niwaombe NaCONGO hakikisheni yale mashirika ambayo hayakuhakiki kwa kipindi cha mwaka mmoja yaeleze sababu kwa nini yasifutiwe ndani ya mwezi mmoja, hapa Iringa ni mashirika 79 kati ya 170″q amesema Mpanju.
Naibu Katibu Mkuu , amesema inatambua mchango mkubwa unaofanywa na Mashirika hayo katika kutekeleza shughuli na huduma mbalimbali kama elimu, afya maji pamoja na huduma mtambuka ikiwemo kusaidia kupambana na ukatili na kuchangia amani na utulivu nchini.
Mpanju amesisitiza kuwa Serikali inafanya uhakiki ili kuhakikisha uratibu wa mashirika unakuwa na ufanisi na pia ni matakwa ya sheria ya nchi na kuongeza kuwa hakuna budi kuratibu shughuli zinazofanywa na NGO kwani kazi wanazofanya ni kubwa.
Wakati huo huo, Mpanju amewaagiza Wasajili wasaidizi wa NGOs kuwapitisha wadau kwenye miongozo mbalimbali ya NGOs ambayo inaeleza namna Serikali na Sekta mbalimbali zinavyoshirikiana ili kufanya kazi kwa ufanisi.
“Nyie wasajili wasaidizi ndiyo wasimamizi wa sekta hii kwa niaba ya Wizara hivyo mnapokuwa na majukwaa kama haya wapitisheni, hakikisheni mwongozo unasambazwa kwani ndiyo unatoa utaratibu mzuri wa namna ya kushirikiana bila migongano” amesisitiza Mpanju.
Kwa upande wao wadau wa NGOs akiwemo Bi Lediana Mng’ong’o kutoka shirika la TAHEA ameshauri mashirika ambayo yalikuwa yamesajiliwa zamani kabla ya usajili wao kuhamishiwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, yafutiwe na yajisajili upya kutokana na changamoto ya kulipa malimbikizo ya nyuma.
Naye Mweka Hazina wa Baraza na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCONGO), John Kiteme amesema baraza hilo linafanya kazi kwa kushirikiana na Serikali kuhakikisha NGOs zinafanya kazi kwa kuzingania sheria na kanuni, ikiwemo mchakato wa kusajili na kufuta mashirika.
Awali akitoa taarifa ya mashirika hayo Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Iringa Saida Mgeni amebainisha kuwa, mashirika yaliyosajiliwa mkoani humo ni 170 lakini yaliyo hai ni 91 na mashirika 79 yanasuasua kutokana na kutotekeleza malengo yao kwa mujibu wa usajili wao na kutokidhi matakwa ya sheria ikiwemo kutolipa ada na kutowasilisha taariza zao za utekelezaji.
“Katika mkoa wa Iringa karibia nusu ya mashirika yana changamoto mbalimbali japokuwa kumekuwa na mafanikio ikiwemo ushirikiano mzuri na wadau wa maendeleo katika kupinga ukatili, kuwasaidia wananchi kiuchumi na kijamii” ameongeza Saida.