Vijana wametakiwa kujikita katika shughuli za uzalishaji mali kupitia fedha za mikopo zinazotolewa na manispaa ya Ilemela na si kujiingiza katika vitendo vya kihalifu kwa kisingizio cha kukosa ajira
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Elias Masalla wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Kawekamo ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kutembelea kata na mitaa ya wilaya hiyo kwa ajili ya kusikiliza kero na changamoto za wananchi, kuzungumza na viongozi wa kata na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa wananchi kupitia kampeni yake ya ‘ONGEA NA DC MTAANI KWAKO’ ambapo amewaasa vijana wa kata hiyo kutoshiriki vitendo vya kihalifu na unyang’anyi kwa kuwa vitendo hivyo huondoa amani na ni uvunjifu wa sheria
‘.. Kukosa ajira kusitufanye tukajiingiza katika vitendo viovu, Ukitenda uhalifu utaadhibiwa kwa mujibu wa sheria hatutaangalia eti umekosa ajira, japo Serikali kila siku inaweka mazingira rafiki ya kujiajiri ..’ Alisema
Aidha Mhe Masalla amewataka viongozi wa dini na wazazi kuendelea kuwalea vijana katika maadili pamoja na kusisitiza wananchi kushiriki zoezi la Sensa ya watu na makazi
Kwa upande wake Naibu Meya wa manispaa ya Ilemela Bwana Sadick Manusura amewataka wananchi wa kata hiyo kuendelea kushirikiana na viongozi wao akiwemo Mbunge Dkt Angeline Mabula na Diwani ili kuharakisha maendeleo sambamba na kumuombea Rais Mhe Samia Suluhu Hassan
Nae Diwani wa kata ya Kawekamo Mhe Omary Bakari mbali na kumshukuru Mkuu huyo wa wilaya Kwa kufika katika kata yake kusikiliza kero za wananchi, amesema kuwa Kamati ya maendeleo ya kata yake inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa soko Nyasaka, ujenzi wa uzio wa shule za msingi Kilimani na Pasiansi, ujenzi wa kituo cha polisi na ujenzi wa vyumba vya madarasa
Ziara ya Mkuu wa wilaya ya Ilemela Kwa wiki la kwanza itahitimishwa katika kata ya Buzuruga kabla ya kuendelea maeneo mengine