WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wanafunzi waliokuwa wanasoma katika vyuo mbalimbali nje ya nchi ambao walirudishwa nchini kufuatia kuzuka kwa janga la UVIKO19 pamoja na kuibuka kwa vita kati ya Urusi na Ukraine wawasilishe taarifa zao Kamisheni ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
Ametoa wito huo leo (Alhamisi, Mei 12, 2022) wakati akijibu swali la Mbunge wa Hai, Saasisha Mafuwe katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Mbunge huyo alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wanafunzi hao kuendelea na masomo wakiwa hapa nchini.
Waziri Mkuu amesema ili kuhakikishia wanafunzi hao wanasaidiwa kumaliza masomo yao wakiwa hapa nchini, Serikali inawataka wawasilishe taarifa zao TCU ambayo imeweka utaratibu unaoruhusu wanafunzi hao kuhamisha viwango vya ufaulu wa masomo vitakavyowawezesha kuendelea na masomo yao nchini.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kununua viuadudu kwa ajili ya kupuliza katika maeneo mbalimbali na kutokomeza mazalia na mbu wanaoambukiza ugonjwa wa malaria. Dawa hizo zinatengenezwa na kiwanda cha Kibaha Tanzania Biotech Product Limited.
Mheshimiwa Majaliwa ametoa agizo hilo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Rose Tweve ambaye amesema Serikali ilifanya uwekezaji mkubwa wa katika kujenga kiwanda cha viuadudu kwa gharama ya wastani wa bilioni 46.
“Wizara ya Afya iliingia mkataba wa kununua dawa hizo na haikufanya kama ilivyokubalika. Je Serikali haioni umuhimu wa kuingia mkataba mpya na kiwanda hiki ili kuweza kununua dawa zitakazo saidia kutokomeza malaria nchini?” amehoji.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kwamba suala la ukarabati wa miundombinu mbalimbali katika shule kongwe nchini ni endelevu na kila mwaka Serikali inatenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa zoezi hilo.
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa jimbo la Mwanga, Anania Thadayo aliyetaka kufahamu Serikali ina mpango gani wa dharura wa kuzifanyia ukarabati shule nyingi ambazo ilizozijenga kwa kipindi kirefu huku baadhi yake zimeanza kuchakaa.