***************************
NA FARIDA SAID, MOROGORO.
Walimu wametakiwa kutumia stadi za maisha katika kuwasaidia wananfunzi wanaorudi shule kupitia mfumo rasmi (reentry) baada ya kusitisha masomo yao kwa muda kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kupata ujauzito kwa watoto wa kike ili waweze kupata elimu na kutimiza ndoto zao.
Hayo yameelezwa mkoani Morogoro na Mkurugenzi wa uthibiti bora wa shule kutoka Wizara ya Elimu Bi. Euphrasie Buchuma wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa walimu kutoka katika Halmashauri tatu za Chemba, Malinyi na Manispaa ya Morogoro.
Alisema kupitia stadi za maisha kutawasaidia walimu kufundisha wanafunzi wengi zaidi kutimiza ndoto zao za kielimu kwani wananfunzi watakuwa wanafahamu namna bora ya kuishi kutokana na mazingira waliopo.
Pia amewahakikishia walimu kuwa Serikali kupitia Wizara ya Elimu na TAMISEMI inatambua mchango wa walimu katika kuleta mapinduzi makubwa ya elimu hapa nchini hivyo itahakikisha elimua ya stadi za maisha inawafikia vijana wengi zaidi kupitia walimu wa unasihi na ushauri nasaha.
Kwa upande wake Mkurugrnzi wa miradi kutoka CAMFED TANZANIA Bi.Nasikiwa Duke alisema mafunzo hayo ya siku tatu yanalenga kuwaongezea maalifa walimu wa stadi za maisha, unasihi na ushauri ili waweze kuwajenga vyema wanafunzi wao wakiwemo wale walioacha shule na kurudi katika mfumo rasmi ( reentry ).
Alisema matarajio yao baada ya mafunzo hayo ni walimu kuja na mpango mkakati wa uwasilishaji wa mafunzo hayo kwa walimu wengine katika shule walizotoka na jinsi gani wanaenda kuimarisha huduma ya unasihi, ushauri, stadi za maisha na malezi kwa wananfunzi wa shule za sekondari.
“CAMFED pamoja na Wizara ya Elimu tuliona ni vyema kutoa mafunzo haya kwa walimu ili yaweze kuwasaidia katika mfumo huu wa reentry ambao ulipitishwa na Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan mwaka jana ambao unawawezesha wanafunzi walioacha shule kurudi kuendelea na masomo yao katika mfumo rasmi.”alisema Bi. Duke.
Mafunzo hayo yameratibiwa na Wizara ya Elimu, TAMISEMI pamoja na CAMFED yamelenga kutoa elimu kwa walimu therathini (30) wa shule za sekondari wa stadi za maisha, unasihi na ushauri kutoka Halmashauri tatu za Malinyi,Chemba na Manispaa ya Morogoro.