Na Dotto Mwaibale, Singida
MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama mkoani Singida wametakiwa
kutoridhika na Sh.Bilioni 1.5 zinazokusanywa kwa mwaka badala yake waongeze
jitihada za kusimamia ukusanyaji ili kuongezeka mapato.
Ombi hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya
hiyo James Mkwega katika kikao cha kawaida cha baraza la madiwani cha robo ya
tatu kilichoketi wilayani humo leo.
Mkwega alisema uhitaji wa bajeti yao ni mkubwa mno
kuliko makusanyo hayo hivyo wasibweteke wakidhani ni fedha nyingi
kwani zipo halmashauri zingine wanakusanya mapato zaidi ya Sh. Bilioni 5 hadi
30 akitolea mfano Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam na kueleza kuwa hata
atapokuwa kwenye vikao vya Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) huwa anachagua wenzake wa kukaa nao wanaolingana katika ukusanyaji wa mapato.
“Ni lazima tukusanye mapato na vyanzo vyetu vipo kwenye
maeneo yenu madiwani tusikubali yakatoroshwa
na kila unapokubali yatoroshwe unajiibia maendeleo kwenye kata yako
hivyo kila mmoja akijihakikishia kulisimamia jambo ili kwa kukaa kwenye mageti
kujiridhidha kama mazao yanayosafirishwa kama yamekatiwa ushuru hasa ya
vitunguu na mengine itasaidia kuiongezea mapato halmashauri yetu” alisema
Mkwega.
Alisema mapato hayo ndiyo yanayoisaidia halmashauri kujenga
vituo vya Afya, Zahanati na miradi
mingine ya maendeleo.
Mkwega aliwaomba madiwani
waliopo kwenye mageti makubwa kusaidia kudhibiti upotefu wa mapato
hayo hasa katika maeneo ya Iguguno, Ibaga, Singa, kidalafa na sehemu
zingine.
Aidha Mkwega aliwahimiza viongozi wa vijiji na vitongoji na
kata kusimamia ukusanyaji wa mapato yanayotokana na madini ya mchanga kwa
kuwaomba Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS)
kushirikiana na vijiji husika unapochimbwa mchanga huo au vifusi kwa
ajili ya kulipa ushuru ambao ni uti wa mapato katika halmashauri hiyo.
Akizungumzia kuhusu zoezi la Sensa ya Watu na Makazi Mkwega
aliwaomba waratibu wa zoezi hilo kuweka nguvu ya kutoa elimu kwa wananchi wa
kabila la Waazabe ambao wapo katika wilaya hiyo ambapo iwapo hawatachukua hatua
za makusudi kulingana na mazingira wanayoishi wanaweza wasipate takwimu halisi
na kujikuta wakikwama.
Hata hivyo Mratibu wa zoezi hilo wilayani humo Daniel Tesha
alimuondoa wasiwasi kwa kumueleza kuwa umewekwa utaratibu mzuri kwa wananchi
hao kwa ajili ya kushiriki zoezi hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo AsiaMessos
aliwahimiza wasimamizi wa zoezi la Anwani za Makazi na Postikodi kuhakikisha
linakamilika kwa wakati ndani ya muda uliopangwa kwani linafanyika ikiwa ni
utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo Lameck Mtungi alitumia
nafasi hiyo kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha mpango wa
kuutangaza utalii wanchi yetu kupitia Filamu ya Royal Tour Tanzania ambayo ilizinduliwa nchini Marekani huku
akisisitiza kuwa huwezi kufanya biashara bila ya kujitangaza.
Mbunge wa Iramba Mashariki Francis Isack aliiomba halmashauri hiyo kuandika andiko
la kuomba ujenzi wa soko la kawaida na la vitunguu litakaloisaidia kupata mapato ambapo pia
aliwapongeza madiwani kwa kazi nzuri
wanayoifanya ya kusimamia miradi ya maendeleo.
Katika baraza hilo madiwani walipata fursa ya kuuliza
maswali ya papo kwa papo na kujibiwa ambapo pia
wenyeviti wa kamati mbalimbali walitoa taarifa ya maeneo wanayoyasimamia
na kuyajadili kwa pamoja.