Watanzania wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho ya siku ya Nyuki duniani ambayo kitaifa yatafanyika katika wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi tarehe 21 Mei 2022 ili kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu umuhimu wa mdudu nyuki katika maisha ya kila siku ya mwanadamu na mazingira yake
Wito huo umetolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Mhe Balozi. Dkt.Pindi Chana (Mb) kwenye taarifa yake kwa waandishi wa Habari Jijini Dodoma.
Waziri Chana ameeleza chimbuko la maadhimisho haya ni azimio la Baraza la Umoja wa Mataifa la Tarehe 20 Desemba, 2017 lililoazimia kuwa tarehe 20 Mei, ya kila mwaka, kuwa ni siku ya nyuki duniani, kwa lengo kuu la kutambua mchango wa mdudu huyu katika kukuza usalama wa chakula na uhifadhi wa mazingira duniani.
“Kufuatia azimio hilo, kila nchi inajukumu la kuadhimisha siku hiyo kuendana na mazingira yake, ili kuendelea kujenga uelewa kwa jamiii juu ya umuhimu wa mdudu nyuki. Na hii ndiyo sababu, sisi kama nchi, tunaungana na dunia kufanya maadhimisho haya kwa mara ya tatu tangu yalipoanzishwa miaka mitano (5) iliyopita” Waziri Chana
Akitaja manufaa ya mdudu Nyuki, Waziri Chana amesema ni pamoja na chakula na dawa, kujipatia fedha za ndani na kigeni, ajiri zaidi ya watu milioni 2 katika mnyororo mzima wa thamani itokanayo na sekta ya ufugaji wa Nyuki.
“Wizara ina mikakati ya kuhakikisha sekta hii inaajiri zaidi ya watu milioni 2.5 ifikapo 2031. Aidha, manufaa yatokanayo na nyuki ni mengi zaidi ya ajira, kwani hata chakula tunachokula nyuki ni sehemu ya wachavushaji wakubwa, na hivyo kutuhakikishia upatikanaji wa chakula”. Aliongeza Waziri Chana
Kauli mbiu ya mwaka huu wa 2022 ni “Nyuki wamehusika: Harakati za kujikwamua upya zisisahau nyuki” (Bee engaged: Build back better for bees). Kauli mbiu hii imekuja kufuatia changamoto ambayo dunia inaendelea kuipitia ya UVIKO 19, na nyuki wamesaidia kwenye mapambani dhidi ya janga hili kwa kuimarisha kinga za miili ya watu.
Pamoja na uwepo wa kaulimbiu hiyo ya kidunia, kaulimbiu ya kitaifa kwa mwaka huu wa 2022, nayo inasema “NYUKI NI UCHUMI: TUWALINDE NA KUHIFADHI MAZINGIRA YAO”. Kaulimbiu hii inaendana na ile ya kidunia kwa kuendelea kuhamasisha wadau kuendelea kutambua umuhimu wa kuwalinda na kuwahifadhi nyuki ili kupata manufaa ya kiuchumi na kiafya.