*******************
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Innocent L. Bashungwa(Mb) amesema kuna haja ya Wizara yake pamoja na Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara kuangalia jinsi ya kuunganisha utoaji wa leseni Kundi A na B ili kuepuka kuwachanganya wafanyabiashara.
Waziri Bashungwa ametoa kauli hiyo alipotembelea banda la BRELA Mei 11, 2022, katika maonesho ya Biashara yanayoendelea mkoani Kigoma.
Mhe. Bashungwa amesema utoaji wa leseni za biashara kundi A zinazotolewa na BRELA na zile za kundi B zinazotolewa na halmashauri zinawachanganya wafanyabiashara.
“Kuna haja ya wizara hizi kukaa pamoja na kuangalia uwezekano utakaowezesha leseni hizi kutolewa sehemu moja tofauti na ilivyo sasa,” amefafanua Mhe. Bashungwa.
Mhe. Bashungwa ambaye amefunga kongamano la biashara na kutoa tamko la kuongeza siku mbili za maonesho yanayoshirikisha wafanyabiashara kutoka nchi za Burundi, Rwanda, Zambia, Congo na Tanzania amesema atazungumza pia na Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA kuhusu jambo hilo.