Baadhi ya wananchi mbalimbali wakipatiwa elimu kuhusu masuala ya Vipimo baada ya kutembelea banda la Wakala wa Vipimo (WMA) kwenye Maonesho ya 5 ya Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yanayoendelea katika uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
************************
NA MWANDISHI WETU
WAKALA wa Vipimo (WMA) wameendelea na utoaji wa elimu ya Vipimo katika Maonesho ya 5 ya Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yanayoendelea katika uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
Akizungumza katika Maonesho hayo leo Mei 11,2022 Meneja WMA Morogoro Bw.Silaji Moyo amesema wapo katika maonesho hayo kwaajili ya kuwawezesha wananchi mbalimbali kuhusu masuala ya vipimo.
Amesema katika banda lao wanatoa elimu kuhusu mizani, mizani hutumika katika maeneo tofautitofauti ambapo kuna mizani ya wafanyabiashara kuuza bidhaa mbalimbali na mizani hiyohiyo hutumika kwenye mabucha kuuza nyama na samaki lakini ipo mizani mingine ambayo inatumika katika barabara ambayo humilikiwa na TANROADS.
“Aina zote za mizani watajifunza katika banda letu na jinsi gani tunahakiki hiyo mizani kwasababu tunapohakiki huwa kuna vitu tunaweka, kwenye vipimo vyote baada ya kuhakiki tukijiridhisha hiyo mizani inapima kwa usahihi huwa tunaweka stika maalumu zenye nembo ya WMA”. Amesema Bw.Moyo.
Aidha Stika ambayo imewekwa baada ya kufanyika uhakiki wa mizani inamthibitishia mtumiaji kuwa hiyo mizani iko salama na imehakikiwa na Wakala wa Vipimo kwaajili ya matumizi husika.
Ameeleza kuwa wanatoa elimu pia jinsi ya kuhakiki vituo vya mafuta ambapo wengi wamezoea kwa jina la sheli huwa tunazihakiki wajilizishe ujazo wa pampu zinazotumika kwenye vituo hivyo vya mafuta kama vipo sahihi.