**********************
Na Mwandiahi wetu, Mirerani
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere, amekagua soko la madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro ili kuona maendeleo ya wafanyabiashara wa madini hayo.
Makongoro akizungumza wakati akikagua masoko hayo amesema serikali imeweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara hao ili wafanye shughuli zao kwa urahisi.
Amesema amepita kukagua kuona namna shughuli za uuzaji na ununuzi wa madini hayo unavyofanyika na kubaini changamoto kama zipo zinazowakabili wafanyabiashara hao.
“Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotoa agizo Tanzanite iuzwe na kununuliwa Mirerani na Rais Samia Suluhu Hassan aliposisitiza hilo inabidi na sisi tusimame kidete kuhakikisha utekelezaji unafanyika,” amesema Makongoro.
Ofisa madini mkazi wa Mirerani, Fabian Mshai amesema shughuli za ununuzi na uuzaji wa madini ya Tanzanite unaendelea kufanyika kama agizo la serikali lilivyotolewa.
Mshai amesema wanunuzi wa madini hayo endapo wakipata changamoto yoyote huwa wanatoa taarifa kwao kama wasimamizi na wanashirikiana nao kuweza kutatua katika biashara zao.
“Wafanyabiashara wa madini ya Tanzanite wanaendelea na shughuli zao bila vikwazo vyovyote kwenye soko la Mirerani na endapo kukiwa na tatizo huwa wanatupa taarifa na tunatatua,” amesema Mshai.
Mkurugenzi wa kampuni ya Tanzanite Forever Lapidary LTD, Faisal Juma Shabhai amesema changamoto iliyopo hivi sasa ni upatikanaji mdogo wa madini ya Tanzanite kutokana na uzalishaji mdogo wa madini hayo.
Faisal amesema wachimbaji madini ya Tanzanite wanapaswa kupatiwa mazingira rafiki ya upatikanaji wa vifaa vya milipuko na vilipuzi kwa urahisi katika migodi yao.
Amesema hivi sasa migodi imechimbwa kwa urefu mkubwa hivyo wachimbaji wanapaswa kuwekewa utaratibu mzuri zaidi wa uchimbaji ili kuondoa gharama kubwa za uchimbaji ikiwemo ankara za nishati ya umeme ambazo ni ghali.
“Dhamira ya dhati ya wachimbaji madini ni kupata uzalishaji ila wanakwama pindi uzalishaji usipofanyika hivyo serikali inapaswa kuwawekea mazingira rafiki zaidi ili wachimbe kwa tija,” amesema Faisal.