Mkuu wa wilaya ya Arusha,Said Mtanda akizungumza wakati akifungua mkutano huo uliofanyika jijini Arusha leo(Happy Lazaro)
Mwenyekiti wa Chama cha waandishi wa habari mkoa wa Arusha ,(APC)Claud Gwandu akizungumza katika mkutano huo jijini Arusha leo.(Happy Lazaro)
******************************
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha.Mkuu wa wilaya ya Arusha ,Said Mtanda amewataka waandishi wa habari mkoani hapa kutekeleza wajibu wao kwa kufuata sheria na kusimamia ukweli na haki katika kazi zao.
Ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati akifungua mkutano kwa waandishi wa habari kwa lengo la kujadili maendeleo ya tasnia ya habari mkoani Arusha hususani katika suala la ulinzi na usalama wa mwandishi,demokrasia na haki za binadamu na wanawake katika uandishi wa habari.
Mtanda amesema kuwa,fani ya uandishi wa habari ni ya muhimu sana katika jamii kwani ina uwezo mkubwa wa kuinua maswala mbalimbali katika.jamii endapo kazi hiyo itafanyika kwa uwazi na uadilifu mkubwa.
“Msiogope kufanya kazi zenu kwenye jamii nyie fanyeni kazi zenu na mkikwama popote mimi nipo tayari kuwapa ushirikiano ama ufafanuzi wowote mnaohitaji ,hivyo lazima mtoe habari kwa wakati ili jamii iweze kuelimika”amesema.
Aidha Mtanda amewataka waandishi wa habari kujiamini katika kutekeleza majukumu yao kwani unapokuwa unajiamini utaweza kukabiliana na changamoto yoyote unayokumbana nayo .
“Popote mtakapopata changamoto ya habari nawaomba Sana msisite kunijulisha ,nawahakikishia mtapata hizo habari kwa wakati,lengo kubwa likiwa ni kuhakikisha haki inafanyika katika upatikanaji wa hizo habari.”amesema Mtanda.
Amesema kuwa, amekuwa akiwashangaa viongozi mbalimbali ambao wamekuwa wakiwaweka ndani waandishi wa habari kutokana na kuandika taarifa mbalimbali ,ambapo amesema kuwa kiongozi yoyote anayefanya hivyo ni kutokujiamini na wengine wamekuwa wakifanya hivyo kwa lengo la kutafuta umaarufu tu.
“Nawaombeni Sana waandishi wa habari kila mmoja aheshimu uwepo wa mwenzake na kwa kufanya hivyo kazi zenu zitaenda vizuri sana bila changamoto yoyote ,na mimi napenda Sana kuwepo changamoto kwani siogopi changamoto kabisa kwani ndo zinazonijenga”amesema Mtanda.
Hata hivyo Mtanda amesema kuwa ,atazungumza na uongozi wa jeshi la polisi mkoani Arusha kuhakikisha kunakuwepo na ushirikiano wa kutosha Kati ya waandishi wa habari na jeshi hilo .
Naye Mwenyekiti wa Chama cha waandishi wa habari mkoani Arusha (APC),Claud Gwandu amesema kuwa,mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo ambayo yamekuwa yakitolewa kwa awamu kwa waandishi wa habari kuhusu kukumbushana katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Gwandu amesema kuwa,maswala ya ulinzi na usalama kwa waandishi wa habari ni muhimu sana kwani ndio kitu cha msingi Sana katika kutekeleza majukumu ya kila siku.
“Mheshimiwa mkuu wa wilaya utendaji kazi wetu na jeshi la polisi mkoani hapa hauridhishi kabisa kwani tumekuwa tukiwaita katika vikao vyetu mbalimbali lakini wamekuwa hawafiki na hatujui shida iko wapi”.amesema Gwandu.
Aidha mkutano huo umeandaliwa na chama cha waandishi wa habari mkoani Arusha(APC) kwa kushirikiana na shirika la Internews na UTPC.