Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia,Prof. Adolf Mkenda ,akizungumza leo Mei 10,2022 jijini Dodoma wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2022/2023.
……………………………………..
Na Alex Sonna-DODOMA
WIZARA ya Elimu,Sayansi na Teknolojia imewasilisha bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka 2022-2023 huku ikiweka vipaumbele katika kuboresha mitaala,elimu ya juu,Mikopo ya elimu ya juu na tafiti.
Akiiwasilisha leo Mei 10,2022 bungeni,Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia,Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali imefanya tathmini ya mitaala 72 iliyowasilishwa na Vyuo vikuu nchini na kutoa ithibati kwa mitaala 31.
Aidha, mitaala 41 iko katika hatua mbalimbali za kupatiwa Ithibati, imeandaa programu saba za masomo kati ya 15.
“Imehuisha programu mbili za mafunzo ili ziendane na uhitaji wa soko la ajira na kuandaa programu mpya mbili kwa lengo la kuongeza wigo wa mafunzo na fursa ya elimu kwa watanzania,”amesema.
MIKOPO YA ELIMU YA JUU
Serikali imeendelea kuongeza fursa za Elimu ya Juu kwa kuboresha huduma za upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini. Lengo la uboreshaji wa huduma ya mikopo ni kuwezesha wanafunzi wenye sifa na uhitaji kuendelea na elimu ya juu bila vikwazo.
Amesema wametoa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 569 kati ya Shilingi bilioni 570 zilizopangwa kutolewa kwa wanafunzi 148,581. Fedha hizo zimetolewa kwa wanafunzi 177,777 kati yao wanafunzi 69,333 ni wa mwaka wa kwanza na wanafunzi 108,444 wanaoendelea na masomo.
“Kipaumbele cha utoaji wa mikopo kimezingatia waombaji wenye uhitaji mkubwa hasa wale wenye ulemavu, yatima na wanaotoka katika kaya maskini zikiwemo zilizopo chini ya mpango wa TASAF,”amesema.
Amesema Bodi imekusanya Shilingi Bilioni 156.806 sawa na asilimia 78 ya lengo la Shilingi Bilioni 201.319 zilizokadiriwa kukusanywa kutokana na mikopo iliyoiva.
“Makusanyo hayo yamechangiwa na mikakati iliyowekwa ya kuelimisha jamii, kuwabaini wanufaika wapya 17,977, utoaji wa ankara za mikopo mipya zipatazo 8,848,”amesema.
TAFITI
Serikali itaendelea kuimarisha uwezo wa ndani wa kufanya tafiti na kutumia matokeo ya tafiti katika kuchangia ajenda ya maendeleo ya Nchi.
“Itafanya tafiti 252 katika maeneo ya mazingira, TEHAMA, nishati, kilimo na chakula, uongozi na biashara, maendeleo ya utalii, sheria, uthibiti wa ubora, utawala na maendeleo, watu wenye ulemavu na mahitaji maalum.
“Maliasili, umaskini, utamaduni, haki za binadamu, maendeleo yawatu na mawasiliano, mifugo, biashara, uvuvi, elimu, sayansi, lugha na fasihi,”amesema.
KUWAENDELEZA WABUNIFU
Amesema Serikali itawaibua, kuwatambua na kuwaendeleza wabunifu na wagunduzi wachanga kupitia Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) kwa lengo la kuwezesha ubunifu wao katika kuchangia kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Amesema wabunifu hao watatoka katika Shule za Msingi na Sekondari, Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi Stadi, Vyuo vya Ufundi, Vyuo Vikuu, Vituo vya kuendeleza teknolojia, Taasisi za Utafiti na Maendeleo pamoja na Mfumo usio rasmi.
KUONGEZA FURSA NA UBORA WA ELIMU YA JUU
Katika kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya juu nchini, Serikali itatekeleza kazi itaratibu udahili wa wanafunzi 133,000 wa mwaka wa kwanza wanaotarajiwa kuomba udahili katika Vyuo vya Elimu ya Juu.
Amesema lengo la kujiunga na programu mbalimbali za masomo kwa ngazi ya Astashahada, Stashahada, Shahada ya Kwanza na Shahada ya Umahiri.
Vilevile, itaanzisha mpango wa fursa za ziada kwa wanawake kwa kuongeza udahili wa wanafunzi wa kike katika programu za sayansi (Science, Technology, Engineering and Mathematics (STEM).
“Itaratibu maombi, uchambuzi na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi 205,893 katika Taasisi za Elimu ya Juu.
Aidha, itafanya ukaguzi kwa waajiri 8,000 kwa lengo la kuwabaini wanufaika wapya takribani 30,000 ili kuwezesha ukusanyaji wa zaidi ya Shilingi bilioni 241 kutokana na mikopo iliyoiva kutoka zaidi Shilingi bilioni 201 za mwaka wa fedha 2021/22.
VYUO VYA UFUNDI
Waziri huyo amesema katika kuongeza fursa za elimu ya ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini, Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji na utoaji wa elimu na mafunzo.
Amesema itasajili vyuo 20 vya elimu ya ufundi na vyuo 80 vya elimu na mafunzo ya ufundi stadi na hivyo kuwa na jumla ya vyuo 538 vya elimu ya ufundi na vyuo 830 vya elimu na mafunzo ya ufundi stadi mtawalia.
“Itahakiki udahili wa wanafunzi takribani 250,000 (vyuo vya Serikali 200,000 na vyuo visivyo vya Serikali 50,000) kupitia Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi,”amesema.
ELIMU YA JUU
Amesema watahakikisha elimu ya juu inayotolewa nchini inazingatia sheria, kanuni, miongozo na taratibu ambapo itafanya ufuatiliaji na tathmini katika Vyuo Vikuu 30 kwa lengo la kuhakiki ubora.
Pia,itafanya tathmini ya tuzo 3,000 zilizotolewa katika Vyuo Vikuu vya nje ya nchi na kuzitambua zitakazokidhi vigezo.
“Itafanya tathmini ya programu 300 za masomo mbalimbali katika Vyuo Vikuu nchini na kuzipa ithibati programu zitakazokidhi vigezo; na itakagua Asasi/Kampuni tano zinazojishughulisha na uratibu wa wanafunzi wanaokwenda kusoma nje,”amesema.
WANAFUNZI WENYE MAHITAJI MAALUM
Amesema Serikali itafanya ufuatiliaji na tathmini katika shule za Msingi, Sekondari na Vyuo vya Ualimu vinavyopokea wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa lengo la kubaini changamoto zilizopo na kutoa ushauri wa kitaalamu.
Pia,itatoa mafunzo kwa wathibiti ubora wa shule 150 kuhusu ufuatiliaji na tathmini ya utoaji wa elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Vilevile,itaendelea kuandika, kuchapa na kusambaza vitabu vya sekondari katika mfumo wa breli na maandishi yaliyokuzwa kwa ajili ya wanafunzi wenye uoni hafifuna wasioona ili kuwawezesha kusoma kwa urahisi.
YAOMBA TRIONI 1.49
Katika Mwaka 2022/2023, Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia imeliomba Bunge kuidhinisha Bajeti ya Sh trilioni 1.49 kwa ajili ya matumizi ya kawaida, mishahara na miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2022/23.