*****************
NA OSCAR ASSENGA,TANGA.
MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeshiriki kwenye mkutano wa 17 wa maafisa habari ,Mawasiliano na Uhusiano wa Serikali mkoani Tanga kwa lengo la kutumia fursa hiyo kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana kwenye mapori ya akiba na Mapori tengefu nchini.
Mkutano huo ulifunguliwa juzi na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye (Mb) ambapo akizungumza wakati wa mkutano huo
alitumia fursa hiyo kumpongeza Mhe. Rais na Amiri Jeshi Mkuu Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za dhati za kufungua sekta ya Utalii nchini.
Pia Waziri huyo aliwataka Maafisa Habari na Mawasiliano kuhakikisha tovuti na mitandao ya kijamii ya Taasisi inatumia fursa hiyo kutangaza vivutio vya utalii na habari nyingine za Taasisi zinazoisemea.
Naye kwa upande wake, Kaimu Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Mahusiano kwa Umma- TAWA ,Twaha Twaibu amesema TAWA inashiriki kwenye mkutano huu kwa lengo kubwa la kuendelea kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana kwenye maeneo yao .
Alisema hiyo ni kama jitihada za kuendelea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan wa kutangaza vivutio nchini kwa kupitia filamu maalumu ya “Royal Tour” iliyozinduliwa hivi karibuni.
Akizungumzia kauli ya Waziri Nape ya kutoa siku 14 kwa Maafisa Habari kutumia tovuti na mitandao ya Kijamii, alisema TAWA imepokea maelekezo hayo na itaendelea kutumia mitandao ya kijamii na tovuti za Taasisi kama nyenzo muhimu ya kujitangaza.
Katika mkutano huo mkubwa umeshirikisha wadau wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kutoka Taasisi mbalimbali za serikali zilizopo Tanzania Bara na Visiwani.