Mmoja wa watoa huduma za Mkoba kutoka Marie Stopes akimuhudumia mteja
*************
Na Irene Mark, Dodoma
SHIRIKA la Marie Stopes Tanzania (MST), limewakutanisha waandishi wa habari zaidi ya 33 jijini Dodoma na kuwapa elimu ya afya ya uzazi na kuwaeleza shughuli zinazofanywa na shirika hilo hapa nchini.
Waandishi hao pia walipata fursa ya kufahamu shughuli nyingine za shirika hilo ikiwemo huduma mkoba ambayo wataalam wa afya kutoka MST huwafuata wananchi wa pembezoni na kuwapa huduma za afya vikiwemo vipimo vya awali na ushauri wa mpango salama wa uzazi.
Akizungumza kabla ya kuanza kwa mafunzo hayo,
Meneja Mawasiliano wa Shirika la Marie Stopes Tanzania, Esther Shedafa alisema shirika hilo lenye matawi bara na visiwani, limedhamiria kuboresha afya ya mtanzania hasa kuhusu afya ya uzazi na huduma za vipimo za saratani.
Shedafa amesema lengo la mafunzo kwa waandishi wa habari ni kupata mabalozi watakaoieleza jamii namna MST inavyofanyakazi mijini na vijijini.
“Kwa upande wa vijana tunakutana nao kwa makundi kupitia majukwaa mbalimbali… kikubwa tunachowafundisha ni afya ya uzazi, kujitambua na kutoa taarifa wanapotendewa ukatili pia tunawahamasisha kufanya ujasiriamali ili kujikwamua kiuchumi,” alisema Shedafa.
Alisema anategemea kuona uelewa wa jamii kuhusu afya ya uzazi na maradhi sugu yasiyoambukiza ikiwemo saratani ambapo MST hutoa huduma za vipimo na nyinginezo kuhusu saratani kwenye vituo na hospitali zao zilizopo Mwenge jijini Dar es Salaam na Mji Mkongwe Zanzibar.
Alitaja maeneo mengine yenye vituo vya afya vya Marie Stopes kuwa ni Kimara Dar es Salaam, Mwanza, Makambako, Iringa, Musoma, Arusha na Kahama.