Ukaguzi wa uwekekaji wa namba za nyumba katika Kitongoji cha Kazikazi wilayani Itigi ukifanyika.
Na Dotto Mwaibale, Singida
KAMATI ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Singida imezitaka Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni na Itigi kuhakikisha zinakamilisha zoezi la anwani za makazi na postikodi hadi ifikapo Jumatano ya wiki hii.
Kamati hiyo ilitoa maagizo hayo jana wakati wakikagua zoezi hilo katika maeneo mbalimbali ya wilaya hizo ambapo kasoro kadhaa zilibainika kuzorotesha kazi hiyo.
“Tunawaombeni ongezeni kasi ya kukamilisha miundombinu ya zoezi ili kwani tupo mbele ya muda uliopangwa hakikisheni vibao vinaanza kuwekwa maeneo yote yaliyoahinishwa” alisema Mwenyekiti wa kamati hiyo wakati akizungumza na maafisa wanaosimamia zoezi hilo wilayani Manyoni ambayo ilibainika kuwa na changamoto kadhaa katika zoezi hilo.
Moja ya changamoto kubwa iliyojitokeza ni utengenezaji wa stika za namba kazi ambayo inafanywa na mzabuni ambaye anakwenda kwa kusuasua hivyo kufikia kuziomba halmashauri hizo kuachana na utengenezaji huo badala yake watumie kuandika ukutani namba hizo kwa rangi ili kuharakisha na kufikia malengo.
Kamati hiyo ilipendekeza nguvu zaidi ielekezwe sehemu za pembezoni na vibao vyenye majina ya mitaa au barabara vitengenezwe kwa ubora ulioelekezwa na si vinginevyo.
Mratibu wa zoezi hilo wilaya ya Itigi Abraham Mfwimi alisema linaenda vizuri katika kata zote na kuwa mpaka sasa wanataarifa 34,553 kwenye mfumo kati ya malengo ambayo yalikuwa ni kaya 35 ambapo utekelezaji huo ni sawa na asilimia 98.7 ya malengo.
Kwa upande wake Mratibu wa zoezi hilo Wilaya ya Manyoni, Emmanuel Mdemwa alisema anwani za makazi walizozikusanya ni 42,680 sawa na asilimia 99.6 huku nguzo za mitaani zikiwa ni 180 na stika 3600 kazi ambayo inaendelea na lengo ni kusambaza katika kata 18 zilizosalia na kuwa usambazaji wa nguzo vijijini wamekwisha peleka nguzo 44.
Alitaja vijiji ambavyo tayari nguzo hizo zimepelekwa kuwa ni Kilimatinde nguzo 3, Sukamahela 7, Chikuyu,Maweni na Kintiko ambavyo hakutaja idadi yake ambapo alisema muitikio ni mkubwa wa kuweka vibao vya majina kwenye taasisi za serikali na mashuleni.
Mratibu wa zoezi hilo Mkoa wa Singida, Athumani Simba aliwaomba watekelezaji wa kazi hiyo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili walielewe vizuri jambo likaloongeza muitikio na kufikia malengo kutokana na umuhimu wake kitaifa.
Baadhi ya vijiji vilivyotembelewa kuona zoezi hilo ni Manyoni Mjini, Kijiji cha Solya, Kilimatinde wilayani Manyoni, Itigi Mjini, Kitaraka na Kazikazi vya wilayani Itigi.