Petro Magai mkufunzi wa mafunzo kutoka Shule kuu ya biashara Chuo kikuu cha Dar es salaam (UDBS)
Wadau wa masuala ya biashara kutoka sekta binafsi na umma wakiwa kwenye mafunzo ya kujengewa uwezo juu ya kuongeza thamani na kupata masoko ndani ya jumuiya ya Afrika mashariki.
Wadau wa masuala ya biashara wakiwa kwenye mafunzo
……………………………………………….
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Kituo cha Biashara cha Kimataifa (ITC) kupitia mradi wa Markup kimetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo Wadau wa masuala ya biashara kutoka sekta binafsi,umma juu ya kuongeza thamani na kupata masoko ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na soko la Ulaya.
Mafunzo hayo ya siku tatu yenye lengo la kuwajengea uwezo wafanyabiashara yameanza kufanyika May 9,2022 katika ukumbi wa Gold crest uliopo Jijini Mwanza.
Akizungumza kwenye mafunzo hayo Mratibu wa mradi wa Markup kutoka kituo cha biashara cha Kimataifa (ITC) Safari Fungo, amesema kuwa mradi huo unatekelezwa na wadau mbalimbali kikiwemo kituo cha biashara za kimataifa ambapo unafanyika chini ya udhamini wa jumuiya ya umoja wa nchi za Ulaya.
“Katika kipindi cha miaka 4 iliyopita tumekuwa tukiwajengea uwezo wataalamu ambao watakuwa wanaendesha semina mbalimbali, baada ya hatua hiyo ulifanyika utafiti mkubwa wa kuangalia ni kwanamna gani taratibu zile ambazo siyo za kikodi zinaleta changamoto kwenye biashara hapa Tanzania ndio maana tulishirikiana na Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara kwa miaka miwili iliyopita hiyo tafiti ilifanyika na ilizinduliwa Aprili 14,2022”, amesema Fungo
Ameeleza kuwa katika tafiti hiyo mambo mengi yalionekana ambayo ni fursa au changamoto kwa wafanyabiashara kuingiza mzigo ndani ya Nchi au kwenda nje ya Nchi.
Amesema miongoni mwa changamoto zilizobainika kwenye tafiti hiyo ni changamoto za vifungashio kuwa shida kwa wafanyabiashara sanjari na uwezo wa wafanyabiashara kuweza kukidhi mahitaji ya soko hasa katika maeneo ya ubora na viwango.
“Baada ya hapo tukaona ni bora watanzania wapate elimu na tumeanza na Mwanza baadae tutaenda Zanzibar na Mbea”,amesema Fungo
Kwa upande wake mkufunzi wa mafunzo hayo wa Shule kuu ya biashara kutoka Chuo kikuu cha Dar es salaam (UDBS) Petro Magai, amesema kuwa elimu ya kibiashara ni muhimu sana ikawafikia wadau mbalimbali ili waweze kujua kila soko la nje linavikwazo vya aina gani.
Elimu hii tunaitoa kwa watu wachache na ndio maana leo hapa Mwanza tumewajengea uwezo zaidi ya watu 30 ili nawao wakawe walimu kwa wengine hali itakayosaidia jamii kuelewa namna ya kuepukana na vikwazo visivyo vya kikodi.
Akizungumza mara baada ya kupewa mafunzo Mwenyekiti wa wavuvi Tanzania Bakari Kadabi, amesema kuwa elimu hiyo imemsaidia kujua mwenendo wa biashara katika Nchi za kigeni ukilinganisha na zamani ambapo alikuwa anakumbana na vikwazo visivyo vya kikodi kutokana na ufinyu wa upatikanaji wa taarifa.
Nae Leopord Lema kutoka Mwanza Quality Wins ameeleza kuwa mafunzo hayo yawe endelevu ili wafanyabiashara wanofanya biashara nje ya mipaka ya Nchi waweze kufahamu ni kwanamna gani wataepukana na vikwazo visivyo vya kikodi.