Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kulia), akisalimiana na Mwenyekiti na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Saruji ya AfriSam, Bw. Erick Diack, nje ya Ofisi za Wizara hiyo (Treasury Square), Jijini Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza na Uongozi wa Kampuni ya Saruji ya AfriSam (hawapo pichani), inayozalisha saruji aina ya Simba. Mkutano huo umefanyika katika Ofisi za Waziri wa Fedha-Treasury Square, Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (wa tano kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe kutoka Kampuni ya Saruji-AfriSam Nje ya Jengo la Wizara ya Fedha na Mipango-Treasury Square, Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akitoa ufafanuzi wa jambo kwa Uongozi wa Kampuni ya Saruji-AfriSam (hawamo pichani) kuhusu namna Serikali ilivyoweka mazingira wezeshi ya uwekezaji.
Mwenyekiti na Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya saruji ya AfriSam, Bw. Erick Diack (kulia), akieleza jambo wakati wa mazungumzo yake na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hayumo pichani). Kushoto kwake ni Mkuu wa Kitengo cha Fedha – Tanga Cement, Bw. Isaac Lupokela na Afisa Mkuu wa Fedha Simba Cement Bw. Pieter de Jager.
Mkurugenzi Mtendaji wa Simba Cement Bw. Reinhardt Swart, akitoa ufafanuzi kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), (hayumo pichani). kushoto kwake ni Mtendaji Mkazi wa Tanga Cement Bw. Benedict Lema ambaye ni nchini kwa Kampuni ya Simba Cement.
Mtendaji Mkazitendaji wa Kiwanda cha Simba Cement Bw. Benedict Lema (katikati), akiongea jambo wakati wa mkutano wa Ujumbe wa Kampuni ya AfriSam na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), (hayumo pichani) kuhusu mkakati wezeshi wa kuendelea kuwekeza Tanzania. kulia kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa Simba Cement Bw. Reinhardt Swart na kushoto kwake ni Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Deni la Taifa, Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Japhet Justine.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango, Dodoma)
************************
Na Benny Mwaipaja, Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ametoa rai kwa kampuni zinazozalisha saruji hapa nchini kuangalia gharama zao za uzalishaji ili kuleta nafuu kwa wananchi pamoja na Serikali inayohitaji saruji kwa wingi katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ya ujenzi.
Dkt. Nchemba ametoa rai hiyo Jijini Dodoma, alipokutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Kampuni ya Afrisam ambayo ni mmoja wa wanahisa wakubwa wa Kiwanda cha Saruji cha Tanga.
Aliishukuru kampuni hiyo kwa kufanikisha upatikanaji wa saruji kwa wakati katika utekelezaji wa mradi wa shilingi trilioni 1.3, Fedha za Uviko 19 na kuwaomba wazalishaji hao kufanya hivyo wakati huu ambapo bei ya vitu vinapanda kutokana na vita vinavyoendelea baina ya Urusi na Ukraine.
Alikumbushia jinsi ambavyo Wizara ya kisekta yaani Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, ilivyokaa na wawekezaji hao wakati wa kujenga madarasa na kuwaomba wasipandishe bei kwa sababu ya uhitaji mkubwa wa bidhaa hiyo uliokuwa umesababishwa na mahitaji ya ujenzi wa madarasa na walikubaliana kufanya hivyo bila kuongeza gharama zaidi.
Dkt. Nchemba alikumbushia pia hivi majuzi pale bei za vifaa vya ujenzi vilipopanda gharama, waliitikia tena wito wa Serikali wa kuwaomba waendelee kuangalia bei ya saruji na kusimamia gharama za uzalishaji.
“Rai yetu, haya mambo ya bei kuongezeka yanaendelea hasa baada ya kuja hili jambo jipya la vita vya Urusi na Ukraine, tuendelee kukabiliana na majanga ya namna hii huku tukiwajali wananchi masikini, sisi huku kwenye sekta ya uzalishaji tukichoka kubeba mzigo, wananchi wetu ambao ni watumiaji wa mwisho watachoka zaidi” alisisitiza Dkt. Nchemba.
Kuhusu masuala ya uwekezaji wao hapa nchini, ambayo ndiyo agenda iliyowapeleka kuzungumza naye, Dkt. Nchemba aliwahakikishia wawekezaji hao kwamba itawalinda na kuwajengea mazingira mazuri ya kufanyabiashara zao kwa kuwa ndio msisitizo mkubwa uliotolewa na Mkuu wa Nchi, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Dkt. Nchemba alieleza kuwa ili kuwezesha uwekezaji mkubwa uendelee kuja Tanzania, ni pamoja na kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji kwa ajili ya kuzalisha ajira na pia vyanzo vipya vya kodi ambavyo vitawapunguzia mzigo na kuwapatia fedha wananchi kwa ajili ya kufanya shughuli za maendeleo.
Kwa upande wake Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya AfriSam, Bw. Erick Diack, alisema kuwa kampuni yake ipo nchini tangu mwaka 1996 na imewekeza zaidi ya dola za Marekani milioni 190.2 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 55.7 kati ya mwaka 2009 hadi mwaka 2016.
Alisema kuwa Kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha tani milioni 1.2 kwa mwaka na katika kipindi kifupi kijacho wanakusudia kuongeza uwekezaji na ufanisi kwa kufunga mitambo mingine yenye uwezo mkubwa wa kuzalisha.