Adeladius Makwega-DODOMA
Jumapili ya Mei 8, 2022 nilikwenda kusali katika Kanisa la Bikira Maria Imakulata Parokia ya Chamwino Ikulu Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma nchini Tanzania.
Misa hii ya Jumapili ya Nne ya Pasaka ambayo pia ni Dominika ya Mchungaji Mwema ilianza saa 12 .00 ya asubuhi ambapo kwa desturi ya kanisa hili husalishwa na Padri Paul Mapalala ambaye ndiye Paroko wa Parokia hii. Lakini siku hii hali haikuwa hivyo misa ilisalishwa na padri mwingine ambaye sikumfahamu jina lake awali.
Baadaye nilibaini kuwa anayesalisha misa hii Padri John Greysoni na kubaini kuwa Padri John Mapalala ni mgonjwa huku akiendelea kupata tahafifu kama alivyosema mwenyekiti wa parokia hii.
Nikiwa kanisa hapo nilibaini Padri Greyson anatoka Shirika la Wamisionari la Damu Takatifu ya Yesu anayefanya utume katika nyumba ya malezi huko Miyuji JImbo Kuu Katoliki la Dodoma.
Misa huku ikiendelea kanisani hapo Padri Greyson aliisoma Injili ya Yohane 10, 27-30. ikiwa injili fupi mno kwa hesabu yangu ya kawaida ilibaini maneno yasiyozidi 45 hata nilipoyaongeza maneno ya awali ya padri huyu na kuitikia kwa waumini hayo maneno yalikaribia 50 tu.
Katika mahubiri yake Padri Greyson alitolea mfano wa Mchungaji Mwema namna anavyowaongoza kondoo wake yeye huwa mbele na kondoo wake wakiwa nyuma. Alikwenda mbali nakusema kuwa namna mchungaji mwema anavyochunga kondoo yeye huwa tayari kwa lolote litakalo tokea liwe baya au nzuri katika uchungaji yake.
“Mchungaji mwema anatoa mwongozo, anatoa dira, anatoa muelekeo na yupo tayari kuwalinda kondoo wake, ana moyo wa ujasiri na yupo tayari kufa kwa ajili yao.”
Ili uwe kiongozi lazima utoe mwongozo, kuwa kiongozi alafu hautoi mwongozo hilo ni anguko kubwa , liwe viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa na hata viongozi wa serikali tunawajibu kutoa miongozo, aliongeza.
Mchungaji huyu hakai nyuma ya kondoo wake na wala hawachapi kondoo wake.Katika mahubiri hayo Padri Greyson alinukuu maneno ya Baba Mtakatifu Frasisco kwa kusema kuwa
“Wachungaji wanapaswa wanuke harufu ya Kondoo”
Maneno haya ya Baba Mtakatifu yanajenga dhana kubwa kuwa Mchungaji Mwema anayechunga kondoo haofii kujitwika begani kondoo wake mathalani aliyeumia, aliyezaliwa machungani na hata aliyemgonjwa.
BInafsi ninasema kuwa Mchungaji Mwema haofii kuchafuliwa mavazi yake na harufu na hata kinyesi cha kondoo wake aliyejitwika begani. Dhana hii inajenga taswira ya viongozi kuwa karibu na wale wanaowaongoza. Hapo ndiyo maana ya wachungaji wanuke harufu ya wanaowangoza.
Dhana hii ya kunuka si dhana ya kunukia manukato bali kunuka harufu mbaya ya si ya mbaya ya mabaya bali ya mfanano na wale walio chini yake, wale walio nyuma yake na wale wanaoongozwa.
Swali ambalo ninaliweka hadharani kwa msomaji wangu ni kuwa je kweli viongozi wetu wananuka harufu ya wanaowaongoza?
Dhana hiyo aliyeiweka mawazoni mwetu Baba Mtakatifu Frasisco ambaye ni kiongozi wa Kanisa Katoliki Ulimwenguni nami kuisikia kupitia kwa Padri John Greyson naiweka kwako msomaji wa matini hii.
“Mchungaji anuke harufu ya kondoo wake.”