Katibu Tawala wa mkoa wa Arusha,Athuman Kihamia akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mtihani wa kidato cha sita yaliyoanza leo (Happy Lazaro).
************************
Happy Lazaro, Arusha.
Arusha.Katibu Tawala wa mkoa wa Arusha,Athuman Kihamia amesema kuwa,serikali ya awamu ya sita imetoa fedha ya uendeshaji wa mitihani kwa ngazi zote na kwa wahusika ambapo jumla ya shs 347,568,000 zimeletwa kwa halmashauri Saba za mkoa huo kwa ajili ya kuendeshea shughuli za mitihani.
Ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya ufanyikaji wa mtihani wa kumaliza kidato cha sita mkoa wa Arusha.
Kihamia amesema kuwa,mpaka Sasa maandalizi yote yamekwisha fanyika na mitihani imeanza na hakuna changamoto yoyote iliyojitokeza ambayo inaweza kuathiri mitihani hiyo.
Kihamia amesema kuwa, idadi ya watahiniwa wote wa shule na wa kujitegemea ni 4,124 ambapo watahiniwa wa shule ni 3,701 na wale wa kujitegemea ni 423 ,huku watahiniwa wa ualimu ni 456 kutoka vituo vinne.
Ameongeza kuwa, idadi ya vituo vya mtihani wa kidato cha sita ni 49 na vituo vya ualimu ni 4,huku idadi ya wasimamizi wakuu wa mitihani ya kidato cha sita ni 49 na ualimu ni 4.
Amefafanua kuwa, idadi ya wasimamizi wa mikondo kwa mitihani ya kidato cha sita ni 121 na ualimu ni 12,huku waandaaji wa mitihani ya vitendo masomo ya Sayansi ni 111.
“kila mmoja wetu anajua kuwa mitihani ya kidato cha sita na ualimu imeanza leo mei 9 na itaisha Mei 27 na maandalizi yote ya msingi yanayotakiwa yalishakamilika na mpaka sasa hivi sijapokea changamoto yoyote kutoka kwa watahiniwa hao.”amesema Kihamia.
“Nikiwa kama Mwenyekiti wa kamati ya mitihani mkoa wa Arusha napenda kuwatahadharisha watahiniwa wote kutojiingiza kwenye vitendo vinavyoweza kutafsiriwa kuwa ni kuhujumu zoezi hili”na wasidhubutu kuingia chumba cha mtihani na vifaa vilivyokatazwa , wasidhubutu kutumia simu au chombo chochote cha mawasiliano kwa ajili ya kusambaza habari za mitihani na wajiepushe na matendo yoyote yanayoweza kuathiri mitihani hi”amesema Kihamia.
Aidha amewataka wasimamizi wote kutanguliza uzalendo na uadilifu kama walivyokula kiapo cha kutunza siri za mitihani,huku akiwataka kuwa watulivu,katika kuepuka papara zinazowakabili kuathiri utaratibu mzima uliowekwa wa ufanyikaji wa mitihani hiyo..