Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Wakili Albert Msando akifungua Maonesho na Siku hiyo ya Ubunifu SUA.
Muwakilishi wa Makamu mkuu wa Chuo ambaye ni Naibu Makamu Mkuu wa huo Pro. Amandus Muhairwa akitoa salamu za Chuo.
Mratibu wa Ubunifu na ushauri wa kitaalamu kutoka SUA Dkt. Doreen Ndossy akieleza chimbuko la Maonesho na siku hiyo ya ubunifu SUA.
Mkurugenzi wa kurugenzi ya shahada za juu Utafiti na ushauri wa kitaalamu Prof. Esron Karimuribo akitoa neno la ukaribisho kwa wageni na washriki,
Mkuu wa wilaya ya Morogoro Mhe. Wakili Albeto Msando akitembelea kazi mbalimbali za wabunifu kabla ya kuzindua rasmi maonesho na siku hiyo ya ubunifu SUA.
*******************
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Wakili Albert Msando amepongeza tafiti zinazofanywa na Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo kwani zinaisaidia Serikali kutengeneza sera bora na kurekebisha zilizopo ili kuboresha namna serikali inavyofanya kazi na kuinua pato la nchi wananchi na taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na Wanataaluma,Wanafunzi,Wabunifu na wadau mbalimbalu wa Chuo kwenye uzinduzi wa siku ya Ubunifu Chuoni hapo iliyofanyika ukumbi wa Freedom square kampasi ya Solomoni Mahlangu Mjini Morogoro.
“Kama hakuna ubunifu maana yake hakuna maendeleo na huwezi kwenda popote, kwahiyo ubunifu ndio jambo linalokaa katikati ya maendeleo kwahiyo niwapongeze sana SUA kwa kuandaa siku hii na kusaidia shughuli za ubunifu ambazo mwisho wa siku bunifu hizi zitakwenda kusaidia taifa letu kupiga hatua za kimaendeleo” alisema Mhe.Wakili Msando.
Ameipongeza SUA kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuzalisha Wahitimu ambao wana mchango mkubwa kwa taifa na kwamba kote aliookutana nao wana mawazo ya kujiajiri na kufungua biashara kwenye kilimo na kufikiria kujiajiri na kuajiri wengine badala ya kutegemea kuajiriwa pekee.
Aidha amesema kuwa changamoto kubwa inayolikabili taifa la Tanzania ni kuwa nyuma sana kwenye masuala ya ubunifu na kwamba bado wapo wengi ambao ni goigoi ambao hawawezi kushughulisha akili zao katika kufikiria na kubuni mambo ambayo sio tu yatamsaidia yeye mwenyewe kwenye Maisha yake ya kila siku lakini pia hata kwa faida ya taifa.
Ameendelea kusema kusema kuwa watu wa chuo kikuu cha Sokoine wanafikiria na ndio maana anapenda kujifungamanisha nao kwasababu ukikaa na watu wenye kufikiri maana unakua na unapata mawazo mazuri mapya kuliko kujifungamanisha na watu wajinga maana ujinga unaambukiza.
Wakili Msando amewataka wabunifu wote nchini kuhakikisha wanatafuta ufumbuzi wa changamoto za msingi kabisa za jamii zinazowazunguka badala ya kufikiria kutatua matatizo makubwa pekee na kujikuta zipo changamoto ndogondogo nyingi ambazo wangeweza zitatua na kuifanya jamii kuishi vyema.
Nae mwakilishi wa Makamu mkuu wa Chuo ambaye ni Naibu Makamu Mkuu wa huo Pro. Amandus Muhairwa amesema Chuo Kimeandaa maonesho hayo ya ubunifu kama sehemu ya utekelezaji wa wa mkakati wa serikali wa kuendeleza na kuimarisha teknoloja na maarifa asilia ya ndani ili yaweze kuchangia katika uchumi wa nchi lakini pia kuhamasisha na kukuza ubunifu na uvumbuzi kupitia sayansi na teknolojia nchini.
“Siku hii ni maandalizi ya mashindano ya kitaifa ya sayansi teknolojia na ubunifu nchini yaani MAKISATU kwa mwa 2022, ambayo huwa yanaandaliwa na wizara ya Elimu sayansi na teknolojia ili kukuza ubunifu wa wazalendo nchini” alieleza Prof. Mhairwa.
Ameongeza kuwa matokeo tarajiwa ya siku hiyo ni kukua kwa hamasa ya ubunifu na kuchochea matumizi ya sayansi na teknolojia katika shughuli za kiuchumi na kijamii ili kufikia hatua ya ubiasharishaji kuchochea ugunduzi wa teknolojia na bidhaa mbalimbali.
Akieleza chimbuko la Maonesho hayo Mratibu wa Ubunifu na ushauri wa kitaalamu kutoka SUA Dkt. Doreen Ndossy ameeleza ni kuibua na kukuza ubunifu ili kuisaidia Serikali katika sekta ya ubunifu hapa nchini.
“Maonesho haya ni sehemu ya maandalizi ya wiki ya kitaifa ya Ubunifu ambayo inatoa fursa kwa Wabunifu,Watunga sera,Wadhamini,Watafiti na wadau wote wa ubunifu nchini kuonesha kazi zao lakini pia kujifunza kwa wengine na kuunda ushirikiano baina yao kwenye sekta mbalimbali ili kuongeza kasi ya kitaifa kwenye matumizi ya teknolojia na ubunifu” alifafanua Dkt. Doreen.
Chuo kimefanya mawasilisho katikata tafiti za kisanyansi,mdahalo pamoja na maonesho ya bidhaa mbalimbali za ubunifu kutoka Chuoni na wadau wengine ambapo lengo la maonesho hayo ni kuchangia juhudi na maendeleo ya kiuchumi.
Siku ya Ubunifu na maoenesho hayo SUA yamebeba kauli mbiu isemayo “Ubunifu kwa mendeleo endelevu” .