*******************
Adeladius Makwega-DODOMA.
Watanzania wametakiwa kuachana na marumbano ya dini na dini na hata dhehebu na dhehebu kwani kushindana huko hakuna tija yoyote kwa taifa letu kwani kila mtu anao uhuru wa kuabudu imani aitakayo.
“Kuna watu bado wanavutana katika misingi ya dini, katika msingi ya kuamini wanagombana na wanakasirikiana kwa sababu mimi ninaamini katika ukristo na mwingine katika dini nyingine na hii inakosesha hata amani ya pamoja kama jamii ya wana wa Mungu.”
Hayo yamesemwa Mei 8, 2022 na Padri John Greyson wa Shirika la Wamisionari la Damu Takatifu ya Yesu anayefanya utume katika nyumba ya malezi huko Miyuji ambaye amesalisha misa ya kwanza ya dominika ya nne ya pasaka na Dominika ya Mchungaji Mwema katika Kanisa la Bikira Maria Imakulata Parokia ya Chamwino Ikulu, Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma.
“Mambo haya hayana afya ya kiroho na kimwili lakini pia yanachochea vurugu, sisi wakatoliki tunasisitiza kuishi kwa amani na watu wa dini zingine, tutembee nao pamoja ndiyo inavyofundisha Sinodi.”
Padri Greyson aliongeza kuwa panapofanyika kazi tabia ya kuharibiana si jambo jema, ni vizuri kufurahia mwezetu anapofanya kazi vizuri na kutokufurahia maendeleo ya mwingine ni roho ya kishetani. Mambo haya yanafanyika makazini, mashambani na hata katika biashara zetu.
“Mtoto wa mwezako anapofanya vizuri kimasomo furahia.”
Padri Greyson alisisitiza kuwa Dominika ya Mchungaji Mwema ina maana kubwa katika maisha ya binadamu hasa kwa kiongozi yoyote kuwa na urafiki wenye afya na wanaongozwa.
Mwandishi wa ripoti hii kwa juma zima ameshuhudia eneo la Chamwino Ikulu likiwa na baridi kali wakati wa usiku na asubuhi, huku jua kali likiwaka mchana kutwa ambalo linasaidia kuyakausha baadhi ya mazao yaliyojaliwa kukomaa kwa sasa mashambani.