NA BALTAZAR MASHAKA,Mwanza
SERIKALI imewashauri Watanzania wenye uwezo na waliowezeshwa na Mungu kupata mafanikio na utajiri,wajifunze kutoa kwa jamii wafanikiwe zaidi.
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Mhandisi Robert Gabriel wakati akipokea msaada wa mgodoro 430 kati ya 1000 yaliyotolewa na The Desk & Chair Foundation kwa ajili ya wafungwa na mahabusu wa Gereza Kuu la Butimba.
Alisema kupitia The Desk & Chair Foundation Watanzania waliowezeshwa na Mungu kupata mafanikio na utajiri wajifunze kutoa sehemu ya mapato yao kusaidia jamii ili wafanikiwe zaidi.
Alisema magereza sio sehemu ya mateso bali chuo cha kurekebisha tabia kwa watu waungwana kufundishwa badala ya kumpa mtu mateso na kuishukuru taasisi hiyo kwa ukarimu wa kusaidia wafungwa na mahabusu vifaa vya kulalia kuwa wamefanya jambo la kiutu.
“Gereza ni sehemu yenye ibanda nzuri,watu wanatulia na hapa Butimba watu walikuwa wakilala chini,walisumbuliwa na ubaridi pamoja na magonjwa ambapo Mungu ameamua kuitumia The Desk & Chair Foundation kusaidia gereza hili,”alisema Mhandisi Gabriel.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Mwanza alisema taasisi hiyo kugusa gereza hilo imeigusa jamii na serikali yoyote duniani haiwezi kugusa maeneo ya magereza na kunukuu maandiko akisema ‘kadiri mlivyowatendea wadogo zangu mlinitendea mimi hivyo tunapotoa baraka tunatengeneza kesho yetu’.
Awali Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation, Sibtain Meghjee akizungumza kabla ya kukabidhi magodoro 430 kati ya 1,000 alisema yote yamegharimu sh. milioni 47 na yametolewa na wadau na wasamaria wema ili kutimiza mahitaji ya wafungwa na mahabusu wa Gereza Kuu la Butimba.
“Tulipokea maombi kutoka kwa Ofisa Magereza Mkoa wa Mwanza, akieleza changamoto yao kubwa ni ukosefu wa magodoro ya kulalia mahabusu na wafungwa,hivyo awali tulikabidhi magodoro 570 na leo (jana) tunakabidhi 430 kukamilisha idadi ya 1,000 ya mahitaji,”alisema.
Meghjee alisema wadau mbalimbali baada ya kuguswa na changamoto ya wafungwa na mahabusu walitoa magodoro hayo na kuahidi kushughulikia changamoto ya maji kwenye gereza hilo kwa kuwachimbia kisima kirefu cha maji.
Mwenyekiti huyo huyo wa The Desk & Chair Foundation alikabidhi magodoro hayo kwa Mhandisi Gabriel ambaye pia alimkabidhi Mkuu wa Magereza mkoani Mwanza, Lazaro Nyanga.