Meya wa jiji la Arusha ,Maxmilian Iraghe akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Arusha, katika ufunguzi wa kongamano la watalaamu wa ununuzi na ugavi lililofanyika jijini Arusha .
Mtendaji mkuu wa PPRA ,Dk. Irene Isack akizungumza katika ufunguzi wa kongamano hilo uliofanyika jijini Arusha .
(Happy Lazaro)
………………………………..
Happy Lazaro, Arusha.
Bodi ya psptb imetakiwa kuwachukulia hatua stahiki za kisheria waaajiri wote wanaokiuka sheria kwa kuwaajiri wataalamu wa manunuzi na ugavi ambao hawajasajiliwa na bodi hiyo kwani ni kinyume na sheria zilizopo.
Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Meya wa Jiji la Arusha, Maximilian Iraghe kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Arusha, John Mongela wakati akifunga kongamano la wataalamu wa ununuzi na ugavi sambamba na wiki ya ununuzi wa umma lililofanyika jijini Arusha.
Iraghe amesema kuwa, kumekuwepo na tabia ya baadhi ya waajiri kutoa ajira kwa wataalamu wa manunuzi na ugavi ambao hawajasajiliwa na bodi ,kitendo ambacho sio sahihi na kwa kufanya hivyo ni ukiukwaji mkubwa wa taratibu na sheria zilizopo.
“Naomba sana bodi ifuatilie swala hili na kuwachukulia hatua wakurugenzi wote ambao wameajiri wataalamu hao ambao hawajasajiliwa ili sheria na taratibu ziweze kufuatwa kama ambavyo bodi inavyoelekeze.”amesema Iraghe.
Amesema kuwa, kisheria hairuhusiwi mtu yoyote kufanya kazi ya ununuzi na ugavi kama hajasajiliwa na bodi ya psptb ,kwani kwa kufanya hivyo ni kinyume na taratibu .
Hata hivyo aliitaka PPRA kuendelea kusimamia vizuri swala la manunuzi ya umma ,huku akiwataka kufanya kaguzi zao katika kuhakikisha wale wote wanaokiuka sheria kushughulikiwa kwa mujibu taratibu zilizopo.
“Naombeni Sana mzingatie misingi ya uadilifu wakati wa kufanya ununuzi huku mkitanguliza uzalendo wa kupenda nchi yenu na ununuzi mnaofanya uendano na kiwango halisi cha fedha hiyo ili kuepuka matumizi mabovu ya fedha za umma.”amesema.
Naye Mtendaji mkuu wa PPRA ,Dokta Irene Isack amesema kuwa,katika kongamano hilo la siku tatu ambalo limeenda sambamba na wiki ya ununuzi wa umma wameweza kuazimia mambo mbalimbali ikiwemo swala zima la uadilifu katika ununuzi ,huku ununuzi huo uhakikishe unaipunguzia gharama ya ununuzi serikali na kuweza kuokoa pesa .
Dokta Irene amesema kuwa,wameweza kuazimia kufanyika kwa tathmini ya kutosha kabla ya kufanya ununuzi ili baadaye waepuke kununua bidhaa mara mbili.
“Tumeweza kuazimia pia kufanyika kwa ununuzi wenye tija na wa gharama nafuu ambao utasaidia watanzania kupata bidhaa na huduma kwa gharama nafuu.”amesema dokra Irene.
Naye Makamu Mkuu wa chuo cha uhasibu Arusha(IAA) ,Dokta Cairo Mwaitete amesema kuwa,manunuzi yanapofanyika mahali popote lazima yazingatie maadili ili yaendane na thamani ya pesa inayotumika.katika manunuzi hayo.
Amesema kuwa ,Kama chuo wamekuwa wakitoa mafunzo kuhusu maswala ya ununuzi unaozingatia maswala ya sheria na taratibu zilizopo, hivyo chuo kimepokea rasmi maelekezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu katika kuhakikisha ununuzi unaofanyika katika maeneo mbalimbali unaozingatia maadili na tayari wao wamekuwa wakifanya hivyo kwa kutoa elimu hiyo kwa vijana wao.