Afisa mifugo Mkoa wa Mwanza akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo leo kwenye kongamano la wanawake wafanyabiashara wa TWCC
Wanawake wafanyabiashara wa TWCC Mkoa wa Mwanza wakiwa kwenye kongamano
Fausta Ntala Mwenyekiti wa chama cha wanawake wafanyabiashara Mkoa wa Mwanza akizungumza kwenye kongamano lililofanyika leo hii Jijini Mwanza
Wakwanza kushoto ni Afisa mifugo Mkoa wa Mwanza Candidah Kyamani akikagua bidhaa za wafanyabiashara wa TWCC Mkoa wa Mwanza
***********************
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Chama cha wanawake wafanyabiashara (TWCC ) Mkoa wa Mwanza wamemuomba Mkuu wa Mkoa huo kuwasaidia kupata mashine ya kuzalisha vifungashio kutokana na malengo yao ya uanzishaji wa kiwanda cha vifungashio.
Ombi hilo limetolewa Leo na Mwenyekiti wa chama hicho Bi,Fausta Ntala wakati wa kongamano la wanawake wafanyabiashara lililofanyika leo May 6,2022 katika ukumbi wa Bwalo la jeshi Jijini Mwanza.
Amesema kuwa kutokana na mazungumzo kati ya Mkuu wa Mkoa na viongozi wa TWCC Mkoa wa Mwanza ya kuanzisha kiwanda cha vifungashio tayari wameshaletewa nyaraka za ununuzi wa mashine hiyo ambayo itagharimu zaidi ya milioni 400.
“Tunaomba sana msaada wako wa hali na mali ili tuweze kufanikisha kupata mashine hiyo itakayotusaidia kuzalisha vifungashio na kukuza uchumi wa chama chetu kwa Mkoa wa Mwanza na Taifa kwa ujumla”, amesema Ntala.
Amesema kuwa mpaka Sasa chama hicho kwa Mkoa wa Mwanza kinawanachama 220, na kimefanikiwa kupata wawakilishi wa bodi ya wakurugenzi wa Kanda ya ziwa kutoka Mikoa ya Shinyanga,Geita.
Akisoma Risala Katibu msaidizi wa chama hicho Jane Ndeto, amesema kuwa lengo kubwa la TWCC ni kuwawezesha wanawake wajasiriamali kupambana kikamilifu katika kukuza uchumi sanjari na kuwawezesha wanawake kuona fursa mbalimbali za kibiashara na kuzitumia kwa lengo la kuwa na biashara endelevu zenye kuleta tija kwa wanawake na kuwajengea uwezo wa kujiamini katika kusimamia biashara zao.
Awali akifungua kongamano hilo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Afisa mifugo wa Mkoa huo Candidah Kyamani amesema kuwa wanawake ni jeshi kubwa sana katika kuleta mapinduzi ya kiuchumi.
Kyamani amewashauri wanawake ambao hawajajiunga na chama hicho wajiunge ili waweze kupata fursa mbalimbali za kibiashara hali itakayosaidia kujikwamua kimaisha.
Amesema kuwa kutokana na ombi walilolitoa kwa Mkuu wa Mkoa ataliwasilisha vyema na anaimani kabisa watapata ushirikiano wa kutosha utakaowezesha kufanikisha kununua mashine hiyo.