Naibu Msajili wa Mahakama ya EACJ,Christine Wekesa akila kiapo mahakamani hapo (Happy Lazaro)
************************
Happy Lazaro,Arusha
Arusha.Naibu msajili wa mahakama ya jumuiya ya Afrika ya mashariki(EACJ) Christine Wekesa ameapishwa leo rasmi katika nafasi hiyo baada ya miaka sita ya kiti hicho kuwa wazi.
Akizungumza leo jijini Arusha katika hafla ya kuapishwa kwa Naibu huyo Msajili wa mahakama,Rais wa mahakama hiyo Jaji Nestor Kayobera amesema kuwa, kiti hicho kilikuwa wazi kwa kipindi cha miaka sita tangu mwaka 2018 baada ya kustaafu kwa aliyekuwa Naibu Msajili wa mahakama hiyo,Geraldine Umugwaneza.
“Christine ndio Naibu Msajili wa EACJ wa pili tangu mahakama ilipoanza mwaka 2001 kwani nafasi hii ilikuwa wazi kwa kipindi cha miaka sita, hivyo tunaamini atafanya kazi nzuri katika kusaidia wananchi waweze kupata,”amesema Jaji huyo.
Ameongeza kuwa, pamoja na kiti hicho kuwa wazi kwa muda mrefu bado wanasubiri nafasi ya Msajili baraza la mawaziri lipitishe ili waweze kufanya kazi kwa pamoja.
Kwa upande wake Naibu msajili wa mahakama(EACJ),Christine Wekesa amesema kuwa, anashukuru kwa kupata nafasi hiyo na anaahidi atafanya kazi kwa ushirikiano ili wananchi wa EAC waweze kupata huduma kwa muda muafaka.
Naye Jaji Mstaafu wa mahakama ya rufaa ya Tanzania,Edward Lutakangwa amesema kuwa, mahakama ni chombo muhimu kinachokuza mahusiano ya kisiasa,kiuchumi na kiutamaduni hivyo kwa kuongeza watenda kazi ni mwelekeo mzuri.
“mahakama ikikosa watenda kazi inaweza kusababisha haki kutopatikana haraka, hivyo nashukuru kwa kupatikana na Naibu msajili wa mahakama hiyo na ni vyema akapatikana Msajili wa Mahakama ili waweze kufanya kazi kwa kusaidiana.”amesema Jaji mstaafu.
“Bila kuwa na Msajili wa mahakama kazi nyingine zaweza kusimama ikizingatiwa kabla ya kesi kumfikia Jaji lazima ipite katika mikono ya Msajili hivyo nasisitiza kwamba muda wote wafuate kanuni za mahakama,”amesema Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa.