************************
Dodoma – Leo, Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt. Donald Wright, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Innocent Bashungwa, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa Bi. V. Kate Somvongsiri wameudhuria uzinduzi wa miradi ya USAID Afya Yangu, yenye thamani ya dola za Marekani milioni 260 ambao ni mpango mkuu wa utoaji huduma za afya katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square mjini Dodoma.
USAID Afya Yangu ni programu ya miaka mitano, inayojumuisha miradi mitatu itakayoshughulikia masuala ya VVU, Kifua Kikuu, Uzazi wa Mpango, Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto na Vijana.
Takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania ina takriban watu milioni 1.7 wanaoishi na VVU, inakabiliwa na changamoto za afya ya uzazi, watoto wachanga na vijana, na inaendelea kuwa na kesi za UVIKO-19 ambazo zimeathiri kwa kiasi kikubwa makundi hatarishi kama vile kina mama wajawazito na watu wanaoishi na VVU.
Serikali ya Marekani imedhamiria kushirikiana na serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika ngazi ya Serikali kuu na mikoa kutoa huduma bora za kinga, matunzo na matibabu ya VVU, Kifua Kikuu na Afya ya Uzazi, Mama, vijana na Watoto ambayo itaboresha matokeo chanya ya afya, hasa kwa vijana, wanawake na watoto.
Programu hii itaboresha lishe na matokeo chanya ya afya katika ngazi ya kaya za Kitanzania kupitia upatikanaji wa huduma bora na kujenga uwezo wa wadau wa ndani kwa ajili ya malengo ya muda mrefu nchini.
Programu ya Afya Yangu inayozinduliwa leo inachangia moja kwa moja malengo haya. Kupitia programu hii, USAID Tanzania itaongeza utambuzi wa watu wanaoishi na VVU na kuhakikisha waendelea kupata matibabu ya kurefusha maisha; na kuboresha uwezo wa watu kujikinga dhidi ya maambukizi ya VVU. Afya Yangu pia itaimarisha mifumo ya afya ya jamii ili kuhakikisha Watanzania katika mikoa lengwa wanapata huduma bora za afya zinazohitajika na kuongeza huduma za uzazi ili kuboresha matokeo ya mimba na watoto wachanga.
Watoto wenye afya njema ndio viongozi wa siku zijazo wa Tanzania wanaoweza kufikia uwezo wao kamili kupitia upatikanaji wa huduma bora za afya na elimu. Serikali ya Marekani imedhamiria kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuendeleza lengo la kuhakikisha vijana wa Tanzania wanakuwa na afya njema, wanaelimika na kupata ujuzi sahihi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi Wright alisema, theluthi mbili ya wa Tanzania wapo chini ya umri wa miaka 25, hivyo ni lazima tuimarishe mifumo ya afya nchini ili kuboresha matokeo ya afya kwa vijana wa Kitanzania ambao wataiongozi nchi hii kuelekea kwenye maisha bora yenye ufanisi thabiti kwa siku zijazo.
Programu ya USAID Afya Yangu utatekelezwa katika mikoa 21 ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa ushirikiano wa karibu na Wizara ya Afya, TAMISEMI, mamlaka za mikoa na serikali za mitaa, asasi za kiraia, Elizabeth Glaser Pediatric AIDS Foundation (EGPAF), Jhpiego, Deloitte na washirika wengine.
Kwa taarifa zaidi, wasiliana na Ofisi ya Mawasiliano Ubalozi wa Marekani kupitia [email protected]