*************
Wakala wa usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imewataka wajasiriamali viziwi kurasimisha biashara zao ili kukidhi takwa la kisheria.
Wito huo umetolewa Mei 05, 2022 na maafisa wa BRELA katika warsha iliyoandaliwa maalum kwa wajasiriamali viziwi kutoka wilaya ya Temeke iliyofanyika ukumbi wa Mbagala Spiritual Center jijini Dar es salaam.
Akiwasilisha mada kuhusu usajili wa majina ya biashara na makampuni, Afisa Usajili wa BRELA Bw. Englibert Barnabas, ameeleza kuwa ni muhimu kwa kila mfanyabiashara kusajili jina la biashara yake kwani vigezo katika usajili ni vichache na itarahishisha wao kutambulika kwa wateja wao na kukuza soko la bidhaa wanazozizalisha na kuuza.
Ameongeza kuwa ili msajili aweze kukubali kusajili jina la biashara ni lazima liwe la kipekee na lisifanane na jina jingine.
Aidha amewataka wadau kutembelea mfumo wa usajili kwa njia ya mtandao wa (ORS) ili kurasimisha biashara zao, na hatimaye kunufaika na fursa mbalimbali zinazojitokeza.
Kwa upande wake Msadizi wa usajili kutoka BRELA, Bi. Yvonne Masele amesisitiza umuhimu wa kusajili alama za bishara na huduma kwani kwa kufanya hivyo kunatoa wigo wa kuendelea kiuchumi na kukuza soko na huduma
Nae Bw. Rajab Chambega. Afisa Leseni kutoka BRELA ameelekeza namna bora za utoaji wa Leseni za Biashara kundi A na Leseni za Viwanda na manufaa yake kwa ujumla.
Bw. Chambega amesema BRELA ipo bega kwa bega na wadau wote ili kuhakikisha elimu hiyo inamfikia kila mmoja huku akiwataka maafisa biashara katika halmashauri husika kuwa msaada na daraja kwa wadau ili kupata elimu ya urasimishaji wa biashara zao.
Nao washiriki wa warsha hiyo wameeleza kuridhishwa na elimu waliyoipata katika warsha hiyo , huku wakiahidi kuwa mabalozi katika ufikishaji wa taarifa juu ya namna bora ya urasimishaji wa biashara, kwa jamii inayowazunguka.
BRELA imedhamini na kutoa mafunzo wa wajasiriamali viziwi lengo likiwa ni kuwajengea uwezo juu ya urasimishaji wa biashara.