Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
WAKAZI wa vijiji katika Kata ya Talawanda ,Jimbo la Chalinze wilaya ya Bagamoyo Pwani, wametakiwa kujikita katika upandaji wa miche ya mikorosho,na kulima kisasa ili kujiwekea hazina ya siku za baadae.
Ramadhani Biga Diwani wa Kata hiyo alitoa ushauri huo kwenye uzinduzi wa upandaji wa zao hilo, limefanyika Kijiji cha Magulumatali, ambapo alisema zao la korosho ni la kibiashara .
Aidha walikagua mashamba yaliyopandwa kisasa akiambatana na viongozi kutoka Halmashauri chini ya Seth Mgonja aliyemwakilisha Ofisa Kilimo, Raphael Kajale ,Ofisa Ushirika na viongozi wengine, Biga alisema kuwa Serikali imeliwekea mkakati zao hilo kwa manufaa ya wakulima wa korosho.
Aliwataka maofisa Kilimo halmashauri kuwa karibu na wakulima, kwa kuwapatia maelekezo sahihi yatakayowasaidia wananchi kunufaika na Kilimo hicho.
“Leo tangu asubuhi tulifanya zoezi la kutembelea mashamba yaliyoandaliwa kisasa na yenye mikorosho bora kiukweli yanaoendeza sana, niwaombe wana-Talawanda tuelekeze nguvu zetu katika kupanda mikorosho, tuipulizie sanjali na kuifanyia palizi,” alisema Biga.
Kwa upande wake Zikatimu aliishukuru Serikali kwa kuwakopesha pembejeo sanjali na mabomba ya kupulizia dawa, na kwamba watakapovuna korosho zao watapeleka katika ghala lililopo kijiji cha Magulumatali, ambalo limejengwa na Serikali.
“Kitendo cha Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wetu Mama Samia kuwakumbuka wakulima kwa kuwakopesha pembejeo na mabomba, inaonesha dhahili ni namna gani inavyowajali wakulimai, tutakapovuna tutazipeleka katika ghala letu,” alisema Zikatimu.
Nae Mgonja alisema kuwa hatua ya Serikali kuwapatia pembejeo na mabomba ya kupulizia inalenga kuongeza ubora wa korosho utaoongeza kipato, huku akiwataka wananchi hao kutokutorosha korosho na kwamba wataobainika watakumbana na mkono wa sheria.
“Hapa tuko na Ofisa Mtendaji na Polisi Kata, hawa viongozi wapo kwa ajili ya ulinzi wetu, lakini niwasihi wananchi tusitoroshe korosho zetu kwa kuwauzia kangomba, atayebainika atakumbana na mkono wa sheria,” alisema Mgonja.
Kajale aliwataka wanaTalawanda kujiunga na chama cha Ushirika kata huku akiwaelezea sehemu ya faida inayopatikana katika ushirika huo ni pamoja na kunufaika na fursa mbalimbali zinazotoka serikalini.