Mfugaji aliyeshambuliwa kwa mishale Masalago Manyenye mkazi wa kitongoji cha Matunduru kata ya Isakamaliwa akiwa amelazwa wodi namba 8 katika hospital ya wilaya ya Igunga mkoani Tabora akipatiwa matibabu
Muuguzi wa hoaspitali ya wilaya ya Igunga mkoani Tabora Magdalena Patrick akimfunika shuka mgonjwa Masalago Manyenye Gamuga mkazi wa kitongoji cha Itunduru kata ya Isakamaliwa anayedaiwa kushambuliwa kwa fimbo na mishale na watu wanane wakati akichunga mifugo yake katika mbuga ya Wembere.
…………………………………………….
Na Lucas Raphael,Tabora
Katika hali isiyokuwa ya kawaida mfugaji mmoja aliyetambulika kwa jina la Masalago Manyenye Gamuga (30) mkazi wa kitongoji cha Matunduru katika kijiji cha Isakamaliwa kata ya Isakamaliwa wilayani Igunga mkoani Tabora amenusurika kuuawa baada ya kushambuliwa kwa fimbo na mishale na kundi la watu wanane wanaodaiwa kuwa nao ni wafugaji.
Akizungumzia Tukio Hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora Richard Abwao alikiri kutokea kwa Tuklio Hilo wachungaji wa Ngombe kungombea sehemu ya malisho.
Alisema kwamba tukio Hilo likitokea Mei 1 mwaka huu majira ya saa 10 Jioni na mpaka Sasa jeahi Hilo linawashikilia watu 6 na linaendelea kuwasaka wengine ambao ndio chanzo za vurugu hizo
Alisema kuwa Jeshi la polisi walifika eneo la tukio na kuwatia mbaroni watu hao sita huku wengine walikimbia baada ya kufanya tukio la kumchoma mwenzao na mkuki ambapo amelazimika kulazwa katika hospitali ya Igunga kwa matibabu zaidi
Hata hivyo akizungumza kwa shida akiwa amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Igunga wodi namba 8 mfugaji huyo alisema tukio hilo limetokea Mei 1/2022 majira ya saa 10 jioni katika Kitongoji cha Matunduru.
Alisema akiwa anachunga mifugo yake ghafla alifikiwa na kundi la wananchi wanane wakiwa na fimbo pamoja pinde zikiwa na mishale ambapo walimsalimia kisha kuanza kumpiga kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili.
Aliongeza kuwa baada ya kuona hali hiyo alianza kupiga kelele za kuomba msaada ambapo baadhi ya wananchi hao aliwasikia wakisema acheni kumpiga na fimbo tumieni mishale ndipo akachomwa mishale miwili shingo na kuelekea kwenye mbavu ya kushoto.
“kwa kweli mimi sijui kama nitapona kwani watu hao wamenijeruhi vibaya sana wamenipiga mshale kwenye mbavu ya kushoto na mshale mwingine kwenye shingo hata hivyo hawakuishia hapo mwingine alinichoma kisu kwenye tumbo nikishuhudia mwenyewe alisema huku akibubujikwa na machozi.
Hata hivyo mfugaji huyo alibainisha kuwa baada ya watu hao kufanya unyama huo walitawanyika kusikojulikana na ndipo yeye mwenyewe aliitoa mishale yote miwili mwilini mwake huku akiendelea kuomba msaada kwa kupiga kelele na ndipo wananchi walifika eneo hilo kisha kumchukua na kumpeleka hospitali ya Igunga.
Nae mmoja wa ndugu zake aliyejitambulisha kwa jina la Mikembo Manyenye anayemuuguza hospitali hapo alisema kata ya Isakamaliwa imekuwa na vurugu kubwa sana ya wananchi kupigwa mishale hovyo ambapo chanzo chake kikubwa ni maeneo ya malisho na kusema kuwa inatakiwa zifanyike juhudi za kutatua mgogoro huo na kuongeza kuwa kwa sasa hana Imani kama ndugu yake atapona hivyo anamwachia Mungu.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Isakamaliwa Dotto Kwilasa (CCM) amekiri kushambuliwa kwa mfugaji huyo na kusema kuwa mgogoro wa Isakamaliwa unatokana na malisho ya mbuga ya Wembere ambapo ameliomba jeshi la Polisi kufanya jitihada za kutatua mgogoro huo kwani umedumu kwa muda mrefu.
Nae mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Igunga Melchades Magongo amethibitisha kupokea mfugaji mmoja Masalago Manyenye Gamuga kutoka kata ya Isakamaliwa akiwa amejeruhiwa vibaya. “Ni kweli tumempokea majeruhi huyo tarehe 01/05/2022 majira saa 2:09 usiku na baada ya kumfanyia uchunguzi tumebaini majeraha makubwa kwenye tumbo na shingo na ubavu wa kushoto na anaendelea na matibabu hali yake siyo nzuri.
Kwa upande wake mkuu wa wiilaya ya Igunga Sauda Mtondoo ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa vitendo kama hivyo serikali haiwezi kuvumilia na wote waliohusikakufanya unyama huo nimeliagiza jeshi la polisi kuwasaka na kuwakamata pia kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Hata hivyo mkuu huyo wa wilaya alitoa wito kwa wananchi pamoja na wafugaji wote kuacha tabia za kujichukulia sheria mikononi na badala yake wanapokubwa na matatizo wayapeleke kwa viongozi wao ili yaweze kutatuliwa kwa taratibu za kisheria.