Mchungaji kiongozi wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Mashariki Ushirika wa Mbezi Luisi Timothy Mwankenja akiwa katika ibada maalumu kusifu na kuabudu iliyofanyika tarehe 1/5/2022 katika kanisa hilo Mbezi Luisi.
Mtumishi wa Mungu Monalisia Swai kutoka Kanisa la KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani Ushirika wa Kurasini akiwa katika ibada maalumu kusifu na kuabudu iliyofanyika tarehe 1/5/2022 katika kanisa hilo Mbezi Luisi.
Waumini wa Kanisa la Moraviani Tanzania Jimbo la Mashariki Ushirika wa Mbezi Luisi wakishiriki ibada maalumu ya kusifu na kuabudu.
…………
Kanisa la Moraviani Tanzania Jimbo la Mashariki Ushirika wa Mbezi Luisi limeanzisha utaratibu wa kuwa na Ibada za Kusifu na Kuabudu kila mwezi lengo likiwa ni kumpa Mungu muda wa kutosha ili aweze kusikiliza shida na mahitaji yao.
Akizungumza hivi karibuni jijini Dar es Salaam baada ya kumaliza ibada Kusifu na Kuabudu, Mchungaji Kiongozi wa Ushirika huo Timothy Mwankenja, amesema kuwa wakristo wanatakiwa kujikita katika sifa kwa Mungu kwa kuwa ndio njia pekee itakayowafanya kuwa baraka kwa familia, Kanisa na Taifa.
Mchungaji Mwankenja amesema kuwa ni vizuri waumini wote wa kanisa la moraviani wapende kumtumikia Mungu. “Ukiipenda ibada Mungu anaonekana na kutupa huduma na maisha yetu yanakuwa na Baraka ndani yake” amesema Mchungaji Mwankenja.
Ameeleza kuwa mtu anayemuabudu Mungu katika roho na kweli anakuwa na faida kwa Taifa pamoja na kanisa kwa sababu anakuwa na hofu ya Mungu kwani anakaa ndani yake.
“Wakati mwengine Mungu anataka tumuabudu kwa muda mrefu, lakini mara nyingi tumekuwa tukisali huku tukiangalia muda kwa ajili ya kukimbizana na majukumu mengine” amesema Mchungaji Mwankenja.
Akihubiri katika ibada hiyo Mtumishi wa Mungu Monalisia Swai kutoka Kanisa la KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani Usharika wa Kurasini, amewahimiza wakristo waliojaliwa vipawa mbalimbali na wanataluma kuzitumia vizuri ili ziwe msaada katika jamii na kanisa badala ya kujibweteka navyo bila faida yoyote.
Amesisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kila mmoja anamiliki ardhi na kuiweka wakfu pamoja na kuzingatia umuhimu wa kumtolea Mungu Sadaka ili kubarikiwa katika shughuli zao.
Ibada hiyo maalumu ya kuabudu na kusifu imeongozwa na neno kuu linalosema inueni vichwa vyenu enyi malango mfalme wa utukufu apate kuingia.